MABASI SABA YAZUILIWA KUENDELEA NA SAFARI MKOANI RUKWA

Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa kupitia kikosi cha usalama barabarani limeyazuia mabasi saba ya abiria kuendelea na safari za mikoani baada ya kukutwa na changamoto katika mifumo mbalimbali.


Mwanasheria wa kikosi cha usalama barabarani nchini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Deusi Sokoni, Disemba 28,2023 akizungumza baada ya kuendelea na zoezi la ukaguzi wa magari, upimaji wa kilevi na utoaji elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abilia katika stendi ya Katumba, alisema jumla ya mabasi 25 yamekaguliwa ambapo kati ya mabasi hayo saba yalikutwa na changamoto katika mifumo na hivyo kuzuiliwa kuendelea na safari. 


Mabasi hayo yaliyozuiliwa ni, kampuni ya Ruchoro Express, Mbinga One express, Mwakamboja, MM8, Bubele trans, Mwasi express, Msigwa trans, yanayofanya safari ndefu kwenda mikoa mbalimbali nchini.


Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama vile Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri Aridhini (LATRA) imepewa mamlaka ya kuzuia chombo cha moto kuendelea na safari pindi linapofanya ukaguzi na kubaini changamoto ikiwemo ubovu au hitilafu katika mifumo ya chombo hicho alisema SSP Sokoni. 


Aidha, Afisa leseni kutoka mamlaka ya udhibiti wa vyombo vya usafiri aridhini (LATRA) Athumani Omary alisema wanafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha abiria waliokuwa wamekata tiketi kwenye magari hayo wanapata usafiri mwingine ili waweze kuendelea na safari zao. 


Naye balozi wa usalama barabarani Mkoa wa Rukwa, Michael Bedeleya alilipongeza zoezi la ukaguzi wa mabasi unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na kuwataka madereva kujenga utamaduni wa kukagua magari yao kabla ya kuanza safari ili kuepuka madhara kwao na kwa abiria wanaowasafirisha.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE