WABUNGE MBEYA WAPELEKA HOJA UWANJA WA NDEGE SONGWE UBADISHWE JINA


 Wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Mbeya wamewasilisha hoja kwa  Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera ili aipeleka hoja hiyo kwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukizi kuomba kubadilishwa jina la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) wakidai kuwa umekuwa ukionyesha taswira ya kuwa  Mkoa wa Songwe na si Mbeya kwa wageni wanaoingia na kutoka.

Mbunge wa Jimbo la Kyela, Ally  Jumbe amesema hayo leo Ijumaa Januari 28, 2022 kwa niaba ya wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Mbeya kwenye kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini hapo kupitia taarifa za miradi  ya miundombinu kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kimsingi uwanja wa Songwe baada ya mikoa kugawanywa ulipaswa kubadilishwa jina na kwamba ni wakati sasa hoja hiyo ichukuliwe na Mkuu wa Mkoa na kuwasikishwa wizarani ili liingizwe kwenye mchakato.

''Pia tutakuwa hatumtendei haki Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini dada yetu Dk Tulia Ackson kwa uwanja huo kuendelea kuitwa Songwe hivyo tuupe hadhi kwani ni mali ya Mkoa wa Mbeya hivyo wakati Mkuu wa Mkoa akilifanyia kazi nasi kama wabunge tutalisemea katika vikao vyetu bungeni '' amesema.

Naye Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka amesema wakati mchakato huo ukiendelea  amelalamikia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kwa kushindwa kutekeleza miradi ya barabara kwa wakati jambo ambalo litaleta hadha kubwa kwa wananchi  na viongozi kukwama wanapokwenda kukagua miradi ya maendeleo.

''Wakati Suala la kubadili jina la uwanja wa ndege likiwa linatekelezwa pia tunaomba Serikali kuweka msukumo kwa wakandarasi wanaopewa miradi kutekeleza kwa wakati kwani mingi imekuwa ikisuasua na kuwa kero kubwa''amesema.

ADVERTISEMENT

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Juma Homera amesema kuwa kuhusu kubadili jina la uwanja huo wabunge wako sahihi kwani umekuwa ukileta mkanganyiko kwa abiria.

''Waheshiwa wabunge hoja yenu ni sahihi mimi nitawasiliana na Waziri mwenye dhamana kulizungumzia hili kwani sioni kama lina ugumu kwani uwanja huo uko katika Mkoa wa Mbeya na ulijengwa kabla ya mikoa kugawanywa ''amesema.

Meneja wa Tanroad Mkoa, Mhandisi  Eliazary Rweikiza amesema miaka ya nyuma walishaanza mchakato wa kulishughulikia suala la kubadili jina uwanja huo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

Amesema atafanya Mawasiliano na Tanroad makao makuu na kupeleka mrejesho ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Juma Homera

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE