MOSHI WAHAHA KUSAKA MAFUTA YAADIMIKA GHAFLA
- Get link
- X
- Other Apps
Siku moja baada ya kuanza kutumika kwa bei mpya za mafuta zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), vituo vingi vya mafuta mjini Moshi vinadaiwa kusitisha uuzaji mafuta kusubiri bei mpya.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital kati ya saa 1 jioni hadi saa 3 usiku leo Jumanne Aprili 5, 2022 umebaini kuwa baadhi ya vituo vilifunga uuzaji wa mafuta saa 12 jioni kwa madai ya kuishiwa nishati hiyo huku baadhi vikikosa huduma hiyo ghafla baada ya bei mpya kutangazwa.
Misururu mirefu ya magari, bajaji na pikipiki ilianza kushuhudiwa saa 12 jioni katika vituo vingi vya kuuza nishati hiyo na baadaye kusitisha huduma kwa madai ya kuishiwa huku taarifa zikidai baadhi vilisitisha kuuza mafuta vikisubiri bei mpya inayoanza kutumika leo nchi nzima.
Kituo cha Oryx karibu na Benki ya DTB kiliendelea kuuza mafuta hadi saa 3 usiku kabla ya kuishiwa huku kituo cha Mount Meru eneo la Majengo kiliuza mafuta hadi saa 4 usiku.
Taarifa iliyotolewa na Ewura ilieleza kuwa bei ya jumla na rejareja kwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara imeongezeka kwamba bei ya rejareja ya petrol imeongezeka kwa Sh285 kwa lita sawa na ongezeko la asilimia 11.12 na dizeli imeongezeka kwa Sh295 kwa lita sawa na ongezeko la asilimia 11.90.
Mjini Moshi lita moja ya petrol ni Sh2,894, dizeli Sh2,825 na mafuta ya taa Sh2,755.
"Kulikuwa na foleni kubwa ya mafuta kwa sababu ya wafanyabiashara wengine kutarajia kupanda kwa bei ya mafuta kesho, ndio maana foleni ipo kubwa na hadi sasa tunasubiri kuweka mafuta,”amesema Steven Paul.
Abuu Yusuph amesema, “Tumekusanyika kwa changamoto ya mafuta ambayo imewakwaza watu wengi katika vyombo vyao vya usafiri, hamna huduma ya mafuta serikali inachukua hatua gani kuhusu ili suala la mafuta, tumekaa takribani masaa matatu hamna mafuta."
Comments