MBUNGE WA MOMBA AINGIA NA GONGO BUNGENI
Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe ameitaka Serikali kuzipima na kuzirasimisha pombe za kienyeji ikiwamo gongo ili kuwasaidia kiuchumi wanawake wanaofanya shughuli hizo
Condester hayo leo Jumatatu Mei 9, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 huku akionyesha baadhi ya baadhi ya pombe za gongo ambazo amesema zimetoka nje ya nchi na zinauzwa hapa nchini.
Amesema hata katika balozi wamekuwa wakitenga fedha kwa ajili ya kununua pombe za bei ghali lakini ukizionja hazina ladha ya tofauti na gongo
“Tunajiuliza ni kwasababu hizi zina jina la kizungu na hizi ni za kibantu. Bodi hii itakapounda itasaidia kwenda kupima viwango vya kilevi vilivyopo.
TBS (shirika la Viwango Nchini), wanaweza kupima wakaondoa makali yaliyoko kwenye gongo ifanane na hizo pombe ambazo matajiri wanakunywa,”amesema mbunge huyo ambaye alikuwa akionyesha aina mbalimbali za pombe.
Amesema biashara hiyo ya pombe za kienyeji wako wafanyabiashara maarufu na wabunge wamesomeshwa na fedha zinazotokana na mauzo ya pombe hizo.
Mbunge huyo amesema wanawake wanaofanya vizuri katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ni wakinamama wanaofanya biashara ya pombe za kienyeji.
“Hatuwezi kudhamini vyetu, hata pombe hatuwezi kuwasaidia hawa watu wapate uthibati (vyeti vya ubora) ?” amehoji.
Hata hivyo, akimpa taarifa Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo alisema kijijini kwake Mgela (mkoani Singida) wamejenga hadi klabu cha pombe ambacho ni moja ya vyanzo vya mapato vya Serikali.
Amesema yeye ni kweli ni mmoja wa wabunge waliosomeshwa kwa fedha zinazotokana na kuuza pombe.
Akiendelea kuchangia, mbunge huyo amesema baadhi ya nchi za nje zimekuwa zikiwasaidia watu wanaotengeneza pombe za kienyeji na kuzirasmisha.
Amesema ili kudhibitisha hilo amefika bungeni na baadhi ya pombe za gongo ambazo zimetoka nje ya nchi na zinauzwa hapa nchini ikiwemo Malawi na Zambia.
Comments