ALIEMZUSHIA KIFO MWAKYEMBE AKAMATWA
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, linamewakamata watuhumiwa wawili kwa makosa ya kimtandao kufuatia msako mkali unaoendelea unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kikosi kazi maalum cha kupambana na makosa ya
kimtandao.
Mtuhumiwa wa kwanza ni Innocent Adam Chengula, Mhehe, 23, mkazi wa Kigogo Luanga, amekamatwa kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Dkt. HASSAN ABBAS Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, kujipatia fedha kwa
njia ya udanganyifu kupitia mtandao na kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.
Mtuhumiwa huyu amekuwa akiweka picha na majina ya Dkt. Hassan Abbas katika maelezo ya ukurasa wake mitandaoni ya kijamii (Profile) na kutuma jumbe kwa watu akiwaomba wamtumie fedha kwenye namba tofauti za simu.
Mfano Amekuwa akituma jumbe zinazosomeka “kaka naomba niazime 3mil alhamis nitakurudishia” na
nyingine “kaka nina mtoto wangu naomba umpatie kazi apo kwako yeye amesomea bachelor of commerce in accounting”.
Aidha pia Jeshi la Polisi limemkamata Tazarn Alfan Mwambengo (27), mkazi wa Ukonga, ambae anatuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu kifo cha Dkt. HARRISON MWAKYEMBE kupitia chaneli ya televisheni ya mtandaoni jambo
ambalo si la kweli.
Katika chanel hiyo ya mtandao mtuhumiwa huyo aliandika “BREAKING NEWS HUZUNI YATANDA MAZISHI YA MWAKYEMBE”. Taarifa hizi ziliibua taharuki kubwa kwa wananchi hasa kwa Dkt Mwakyembe mwenyewe na familia yake.
Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:
1. Kompyuta mpakato (laptop)1
2. Simu 3,
3. Mike ya kutangazia,
4. Modem 1,
5. Kadi za simu za mitandao mbalimbali 9 zenye usajili wa majina tofauti.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Watanzania kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa zitakazo zua taharuki kwa umma, pia linawaomba watanzania kuchukuwa tahadhari wakati wa kutuma pesa au kufanya miamala kwa njia ya simu ili kuepuka kutapeliwa, Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa watu wote watakao vunja sheria, kanuni na miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya mitandao.
Comments