DC GODIGODI AAGIZA MMILIKI WA SHULE KUKAMATWA BAADA YA KUMPELEKA MWANAFUNZI WA KIKE POLISI KWA KUSHINDWA KULIPA ADA
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Hanji Godigodi ameliagiza Jeshi la Polisi kumkamata mmiliki wa shule ya sekondari Kaozya Mlimba kwa madai ya kumpeleka kituo cha polisi mwanafunzi wa kidato cha nne baada ya mzazi wa mwanafunzi huyo kushindwa kulipa ada ya muhula wa pili wa masomo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Septemba 24, 2022, Hanji amemtaja mmiliki wa shule hiyo kuwa ni, Erick Kaozya na kubainisha kwamba Serikali imetoa miongozi mbalimbali ya elimu kwa shule za msingi na sekondari juu ya uendeshaji wa shule hizo.
“Kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na maelekezo ya serikali, mwanafunzi haruhusiwi kurudishwa nyumbani au kufukuzwa shule kwa sababu mzazi kukosa ada hasa kwa madarasa ya mitihani ya darasa la nne na la saba lakini hata kidato cha pili, nne na kidato cha sita,” amesema Hanji
Hata hivyo, mkurugenzi wa shule hiyo, Erick Kaozya amesema si yeye aliyempeleka mwanafunzi huyo polisi bali ni kaka wa mwanafunzi ndiye aliyemwambia aende polisi bila kufafanua sababu za kupelekwa polisi.
“Mimi sihusiki kumpeleka mwanafunzi kituo cha polisi, isipokuwa ni kaka wa huyo mwanafunzi ndiye aliyempeleka kituo cha polisi,” amesema Erick.
Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 amesema kabla ya kupelekwa kituo cha polisi, tayari alikuwa amefukuzwa shule baada ya kutoelewana kati ya mzazi wake na mkurugenzi hiyo.
“Mzazi wangu alituma ada katika namba ya simu ya shule na alipowajulisha ametuma fedha kwa njia ya simu, alijibiwa hawajaona muamala na mzazi wangu alisitisha muamala ili fedha irudi na itumwe kwa njia nyingine…, shida ilianzia hapo,” amesema mwanafunzi huyo.
Amebainisha kwamba huenda chanzo kingine cha kufukuzwa shule si ada bali ni kuhoji sababu za wanafunzi wa kike kupangiana zamu ya kupika chakula wakati shule imeajiri mpishi
Comments