KUMBUKUMBU YA MAISHA YA MH. ESTER ALEXANDER MAHAWE
Tarehe ya Kuzaliwa: 05 Novemba, 1973
Mahali: Kijiji cha Isale, Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara
ELIMU
Mh. Ester Alexander Mahawe alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi Upper Kitete, Wilaya ya Karatu mnamo 1982-1983 na baadaye kuhamia Shule ya Msingi Isale, ambako alihitimu mwaka 1988.
Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Imboru, Wilaya ya Mbulu kati ya mwaka 1989-1992.
Mnamo 1994-1996, alihitimu mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka Chuo cha Ualimu Monduli, Mkoa wa Arusha.
Mwaka 2012-2013, alihitimu stashahada ya Uongozi na Utawala kutoka Chuo cha ESAMI, Mkoa wa Arusha.
NDOA NA FAMILIA
Mnamo tarehe 17 Septemba 2005, Ester Alexander Mahawe alifunga ndoa na Alexander Samson. Ndoa yao ilijaliwa watoto watatu wa kuwazaa: wavulana wawili na msichana mmoja. Aidha, aliwalea watoto wengine sita na hivyo kuacha jumla ya watoto tisa pamoja na wajukuu tisa.
KAZI NA UZOEFU
Huduma ya Ualimu:
1996-1997: Mh. Ester alikuwa mwalimu katika St. Constantine International School, Arusha.
1997-1998: Alikuwa mwalimu mwanzilishi wa Shule ya Trust St. Patrick Schools, Arusha.
1998: Alianzisha shule binafsi ya awali na msingi iitwayo Jue Pre and Primary School iliyoko Sakina, Arusha.
Mafanikio ya Uwekezaji:
Mnamo 2012, Ester na mumewe walizindua Intel Schools iliyopo Muriet, Arusha, ambayo kwa sasa inatoa elimu ya awali, msingi, na sekondari.
Huduma ya Kisiasa na Kijamii:
2015-2020: Alikuwa Mbunge wa Viti Maalum akiwakilisha Mkoa wa Manyara. Alijulikana kwa juhudi zake za kutetea haki za wanawake, vijana, na makundi maalum.
2015-2020: Rais wa Jumuiya ya Wawekezaji Binafsi katika Sekta ya Elimu Tanzania (TAPIE).
2018: Mjumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Tanzania Rift Valley Field (Kanisa la Waadventista Wasabato).
Alishiriki kwa karibu katika miradi ya maendeleo ya elimu na afya kwa kushirikiana na wananchi wa Babati.
Uongozi Ndani ya CCM:
2015-2020: Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara.
2021-2022: Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa Jimbo la Babati.
Uteuzi wa Mkuu wa Wilaya
Juni 2021: Mh. Ester aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma.
2023: Alihamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, alikohudumu hadi mauti yalipomfika.
MAPAMBANO NA MARADHI
Mnamo Agosti 2023, Mh. Ester aligunduliwa kuwa na maradhi ya saratani. Alipata matibabu katika hospitali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
Bangalore na Apollo nchini India,Ocean Road, Muhimbili, na Lugalo jijini Dar es Salaam,KCMC, Moshi.
Mnamo tarehe 13 Januari 2025, akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Lugalo, hali yake ilibadilika na alihamishiwa KCMC. Tarehe 14 Januari 2025, majira ya saa moja na nusu asubuhi, alifariki dunia akiwa KCMC, Moshi.
URITHI WAKE
Mh. Ester Mahawe ameacha mume, watoto tisa, na wajukuu tisa. Atakumbukwa kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu, kutetea haki za wanawake, na kusukuma mbele maendeleo ya jamii alikohudumu.
MWISHO WA SAFARI YA MAISHA
Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mh. Ester Alexander Mahawe. Ametuachia urithi mkubwa wa upendo, juhudi, na uongozi bora.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Comments