MWALIMU AFUNGWA KIFUNGO CHA MAISHA MARA 2 NA MIAKA 30 JUU KWA KULAWITI



 Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma mkoani Mara, imemuhukumu kifungo cha maisha jela mwalimu Idrisa Athumani (29) wa shule ya Msingi Kyawazaru iliyopo wilayani Butiama baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake (14).

Hukumu hiyo iliyotolewa leo Ijumaa Septemba 23, 2022 ni ya tatu kutolewa dhidi ya mwalimu huyo ambapo hukumu ya kwanza ilitolewa Septemba 14, mwaka huu na Mahakama ya Wilaya ya Musoma mwalimu huyo alihukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mara mbili mwanafunzi wake mwingine.

Hukumu ya pili ilitolewa Septemba 16, 2022 na Mahakama hiyo hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake mwingine (12).

Hukumu ya tatu imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Stanley Mwakihaba baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo dhidi ya mashataka yaliyokuwa yakimkabili mwalimu Athumani.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mwakihaba amesema mwalimu huyo amefanya kosa hilo kinyume cha kifungu namba 154 kifungu kidogo cha kwanza (a) na cha pili cha Kanuni ya Adhabu Sura Namba 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Amesema mwalimu huyo alifikishwa mahakamani hapo Julai 20, 2022 na kufunguliwa kesi namba 52. Katika shauri hilo jumla ya mashahidi wanne walitoa ushahidi wao akiwemo daktari aliyemfanyia vipimo mtoto huyo.

ADVERTISEMENT

"Mahakama inakuhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa sheria na adhabu hii inatolewa ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya vitendo kama hivi " amesema

Hakimu huyo amesema kuwa kwa mujibu wa maelezo na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo mwalimu huyo alimlawiti mwanafunzi huyo wa darasa la sita mara tano kwa nyakati tofauti kati ya mwezi Januari, 2021 hadi Februari 2022.

 "Baada ya vitendo hivi kubainika ndipo hatua zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kupelekwa polisi na kisha kufikishwa mahakamani Julai 20 kwa ajili ya hatua zaidi" amesema

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mojica Hokororo.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE