SONGWE KILIMO CHA MBOGAMBOGA, MATUNDA CHAHIMIZWA SHULENI
Na Baraka Messa, Songwe.
KIKAO Cha Kamati ya lishe Mkoa wa Songwe, kimeazimia Shule zote za Msingi na Sekondari kuanza kupanda Bustani za mbogamboga na matunda Ili kuimalisha lishe kwa watoto.
Kamati ya Mkoa imetoa pendekezo hilo wakati wa kikao cha robo cha lishe kupitia utekelezaji wa Afua za lishe kilichofanyika juzi katika Ukumbi wa Mkoa wa Songwe.
Mjumbe wa Kamati hiyo Charles Chenza alishauri kamati kuweka azimio la kuitaka kila shule ipande miti ya matunda kama maparachichi, maembe kulingana na hali ya hewa ya eneo la shule ilipo, pamoja na Bustani ya mbogamboga kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
Naye mwakilishi wa Kamati ya Amani Mch. Rogers Simkonda amesema jamii imekuwa ikipuuza suala la kulima mazao na bustani majumbani mwao na hata kwenye taasisi kama mashule na kuacha maeneo wazi.
"Kwenye taasisi zetu kama mashule hakuna jitihada za kuzalisha chakula kwa ajili ya chakula cha mchana lakini hayo hayafanyiki na hata mazao kama migomba iliyopandwa kwenye maeneo hayo imeanza kuharibika na hakuna ufuatiliaji" amesema Simkonda.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda alisema licha ya Mkoa wa Songwe kuwa moja ya mikoa inayozalisha chakula kwa wingi lakini ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na udumavu unaosababishwa na lishe isiyozingatia ulaji bora wa makundi matano ya vyakula,
Alisema Mpaka sasa mkoa wa Songwe ambao ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi mazao ya chakula udumavu kwa watoto uko asilimia 43.3 Kitaifa.
"Ukosefu wa lishe bora kwa Mtoto ni hatari kwa maisha yake na jamii, hivyo tujitahidi siku 1,000 za mwanzo tuimarishe lishe ikiwemo kuhakikisha mama mjamzito anapata lishe bora na mtoto naye" alisema Seneda.
Amesema kuanzia sasa ulimaji wa Bustani na upandaji wa miti ya matunda upewe kipaumbele Ili kumjengea mtoto tabia ya kulima mbogamboga na matunda tangu akiwa mdogo chini ya miaka nane shuleni.
Comments