WATUMISHI 5 HALMASHAURI WASIMAMISHWA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amewasimamisha kazi maofisa watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara kwa kusababishia hasara na matumizi mabaya ya madaraka.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Juma Mavumo, aliyekuwa Kaimu mweka hazina Ramadhan Mwakamyanda, Mweka Hazina wa sasa Respicius Kagaruki na Mkuu wa Kitengo cha Tehama Nyanda Msirikale.
Bashungwa amesema watumishi hao wamesimishwa kulingana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21.
Pia Mhasibu wa Mapato, David Assey amesimishwa kazi kutokana na kukopa fedha Sh6.7 milioni kwa ajili ya matumizi ya ofisi na kuzipeleka kwenye akaunti binafsi.
Bashungwa ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 28, 2022 baada ya ziara ya siku mbili mkoani Manyara.
Amesema taarifa ya ukaguzi wa kawaida kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 iliagiza Mvumo achukuliwe hatua stahiki kwa kushindwa kuandaa vyema masharti ya zabuni.
Amesema pia taarifa hiyo imeonesha Mwakamyanda na Kagaruki wachukuliwe hatua kwa kulipa gharama za uwakala kwenye akaunti ya binafsi badala ya akaunti ya kampuni M/S Dicsamo Traders iliyopewa zabuni ya kukusanya mapato ndani ya halmashauri kiasi cha Sh188.49 milioni.
Amesema CAG pia ilielekeza Msirikale na Kagaruki wachukuliwe hatua kwa kushindwa kusimamia vyema Mfumo wa Mapato na kuacha mashine za kukusanyia mapato kuendelea kuwa nje ya mtandao kwa kipindi kirefu cha kati siku 8 hadi siku 1,051 (takribani miaka 3) bila ufuatilia.
Waziri huyo amesema Julai 12, mwaka huu, aliyekuwa anakaimu ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mbulu, David Assey aliandika barua kwa kampuni binafsi ya kukopa kiasi cha Sh6.7 milioni kwa aijli ya matumizi ya ofisi na kisha kuelekeza fedha hizo kuwekwa kwenye akaunti yake binafsi.
Aidha, Bashungwa ameyataka mabaraza ya madiwani kuacha tabia ya kuwasamehe watumishi waliotakiwa na CAG kuchukuliwa hatua.
Comments