SHERIA YA KILIMO KUTUNGWA
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, amesema serikali ipo njiani kutunga sheria maalum kwa ajili ya kilimo ili kulinda maeneo yote yanayofaa kwa kilimo katika azma yake ya kukuza sekta ya kilimo nchini.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ihus Bariadi mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya ardhi ya vijiji 975 walipofika katika eneo hilo.
"Katika kulinda maeneo yanayofaa kwa kilimo na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi nchini, serikali kupitia wizara ya kilimo tunaendelea na hatua za utungwaji wa sheria ya kilimo, kwa kuwa dhamira yetu kubwa ni kuhakikisha tunakuza sekta hii ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hatua hii lazima iende sambamba na kuyatambua maeneo ya kilimo na kuyalinda kisheria," amesema Mavunde
Kwa mujibu wa Mavunde katika maeneo yote ya utatuzi wa migogoro ardhi inamegwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na kutaka mamlaka za upangaji wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo husika kuhakikisha zinatenga maeneo ya mashamba makubwa ya pamoja ya kilimo (block farms) ili serikali iweze kuwahudumia wakulima kwa urahisi.
Comments