Songwe kuongeza elimu unawaji mikono kujikinga na magonjwa ya tumbo na milipuko
Na Baraka Messa, Mbozi.
MKUU wa Mkoa wa Songwe Waziri Kindamba ametoa rai kwa viongozi wa afya mkoa na katika Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe kuongeza kasi ya kutoa limu ya unawaji mikono ili kujikinga na magonjwa ya tumbo ambayo yanauathiri Mkoa pamoja kujikinga na magonjwa ya mlipuko .
Mkuu wa Mkoa Kindamba amesema hayo hivi karibuni katika maadhimisho ya siku ya unawaji mikono ambapo kimkoa yalifanyika katika kijiji cha Mbozi kata ya Igamba wilaya ya Mbozi mkoani hapa.
Alisema mko wa Songwe haufanyi vizuri katika suala la unawaji mikono , Uharibifu wa Mazingira na ujenzi wa Vyoo bora, hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya tumbo na milipuko kama vile kipindu pindu, korona na Ebora.
‘’Mkoa wetu unashika nafasi ya 17 kitaifa katika suala zima la unawaji mikono , ambapo kaya zenye vifaa vya kunawa mikono katika vyoo ni asilimia 35, wakati wastani wa unawaji mikono kitaifa ni asilimia 41, Mikoa mitatu inayoongoza kwa kuwa navifaa vya kunawia mikono ni Iringa asilimia 77, Njombe asilimia 73.9 na Kilimanjaro asilimia 73.5 “ alisema Kindmba.
Aliitaja halmashauri ya mji Tunduma kuwa ipo chini zaidi kwa kuwa na asilimia 17, nyingine ni Songwe asilimia 27, mbozi 36 Ileje 39 na Halmashauri ya Momba asilimia 44, alisema kutokana na takwimu hizo mkoa una kazi kubwa ya kufanya kwa viongozi wakishirikiana na wananchi katika halmashauri kuwa na mipango ya kuhakikisha tunakuwa na vyoo bora sambamba na vifaa vya kunawia mikono katika kaya , shule na maeneo mbalimbali zinapofanyika shughuli za maisha.
Kaim Katibu tawala mkoa wa Songwe Boniface Kasululu alisema malengo ya mkoa ni kuongeza kiwango cha kaya zenye vyoo bora kutoka asilimia 78 hadi kufikia asilimia 100 na kuongez kiwango cha kaya zenye vifaa vya kunawa mikono kutoka asilimia 35 hadi kufikia asilimia 50 ifikapo disemba 2023.
Kwa upande wake Afisa mabadiliko tabi ya jamii kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Communication and Development Center (TCDC) Gaston Gration alisema kuwa magonjwa mengi ya tumbo na kuhara wanayoumwa wanachi wa Songwe yanatokana na uchafu wa kutokunawa mikono sambamba na uchafu pamoja na uharibifu wa mazingira.
Alisema wakishirikiana na mkoa wa songwe wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kufikia juni mwakani 2023 kuhakikisha wagonjwa wanaoumwa mgonjwa ya tumbo na kuhara yanayosababishwa na ulaji uchafu hasa kinyesi yanakomeshwa kabisa katika mkoa wa Songwe.
Kwa upande wao wananchi wanasema kuwa unawaji mikono uliongezeka zaidi kipindi ambacho maambukizi ya ugonjwa wa korona yalikuwa juu kwa sababu viongozi walikuwa wanahamashisha sana swala la unawaji mikono.
Mkazi wa kijiji cha Mbozi Misheni Kendy alisema hamasa ya kunawa mikono imepungua hivi sasa ukilinganisha na miaka miwili ya nyuma kutokana na hamasa kupungua kwa wananchi, hivyo kuona kama sio jambo la lazima.
Naye ni mfanyabiashara katika kijiji cha Matula Upendo Mwanjila alisema licha ya kuweka ndoo na maji ya kunawa Bado baadhi ya watu hawataki kunawa mikono wanapoingia dukani au kutoka chooni.
Comments