JOYCE MWAZEMBE; MLEMAVU ANAYETEMBEA KWA KUTAMBAA , MWENYE NDOTO ZA KUSAIDIA WALEMAVU, YATIMA NA WASIOJIWEZA
Na Baraka Messa
"NILIANZA na mtaji wa shilingi 18,000 ambao nilipata baada ya mama angu mzazi kwenda kuniuzia mnadani Vwawa viazi vichache nilivyovivuna ambavyo nililima nyumban.
Mama alipo Rudi na kunikabidhi hela aliyoniuzia viazi nilifurahi sana, nilinunua karanga za maganda debe tatu nikazimenya nikapata debe moja la zilizomenywa nilipoliuza nilipata shilingi 21,000 niliendelea na biashara Hiyo ya karanga baadae mtaji ulivoongezeka nilianza kununua samaki" anasimulia Joyce Alan Mwazembe (36) ambaye ni Mlemavu wa miguu anayepata mahitaji yake kwa kutambaa .
Joyce ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Sumbaluwela Kata ya Ihanda Wilaya ya Mbozi anasema ulemavu alionao hakuzaliwa nao bali aliupata akiwa na umri wa miaka 15 akiwa darasa la tano katika shule ya Msingi Sumbaluwela.
Akiongea na mwandishi wa makala haya aliyemtembelea Kijijini hapo, anasema ulemavu wake aliupata baada kudondoka kwenye mti wakati akijaribu kuchuma matunda aina ya parachichi, ambapo anadai kuwa alipo dondoka alizimia na kuzinduka akiwa hospitalini Vwawa ambayo ni hospital ya Wilaya ya Mbozi.
"Maumivu makali niliyopata, Lakini chakushangaza nilipochukuliwa vipimo vya mionzi madaktari walidai nmepata mshitiko tu viungo viko vizuri niendelea kupata maumivu makali ndipo walipo nihamishia hospitali ya Mbozi Mission nako baada ya vipimo walinambia majibu yanayofanana na hospitali ya Vwawa
Baada ya muda niliandikiwa Rufaa ya kwenda kupata matibabu hospitali ya Rufaa Mbeya ambayo ni ya kandaa Nako baada ya vipimo walidai sijaumia sana waendelee kunifanyisha mazoezi" anasema Joyce.
Anasema baada ya mwaka mmoja alianza kuinuka Lakini miguu iligoma kabisa na Hivyo kushindwa kutembea Wala kusimama.
" Ilinilazimu kuanza kutembea kwa kutambaa , niliumia sana na kuona ndoto zangu zote kufutika kichwani mwangu" anaeleza kwa machungu Joyce huku mchozi yakimtoka.
AANZA KUFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO
Anasema mtaji wake wa karanga ulipoongezeka alianza kujumua samaki na kuuzia nyumbani, huku faida akiitumia kwa ajili ya kulima mahindi kwa ajili ya chakula ambacho wanakitumia na mama yake mzazi ambaye naye ni mgonjwa wa muda mrefu kwani huwa anasumbuliwa na kifua.
Anasema alipata mafunzo kidogo ya ujasiriamali kutoka shirika la Stryde ambalo lilikuwa linawafundisha vijana ujasiriamali.
Anasema alijifunza namna ya kuhifadhi pesa hata kama ni kidogo ambapo akiba hiyo ilianza kumnufaisha kwani aliweza kununua kidogo mbolea na mahitaji mengine ya nyumbani, kwa kuwa yeye ndiye anayetegemewa na familia yao kwa mahitaji muhimu ya chakula, maradhi na mavazi kwani mama yake na mtoto mmoja yatimaa ambaye wazazi wake walifariki wanamtegemea
"Baba alifariki mimi nikiwa mdogo kabisa ,watoto tulizaliwa wanne lakini saizi tumebaki watatu mimi kaka yangu na mdogo wangu kiume, hawa ndugu zangu wote wameoa wanajitegemea, mama anakaa na mimi pamoja mjukuu awake ambaye ni mtoto wa mdogo angu wa kike aliyefariki na Mme wake hivyo kumwacha mtoto mikononi mwa mama " anasema Joyce.
Anasema mama yake ni mdhaifu muda mrefu, anasumbuliwa na kifua huwa hana uwezo wakufanya kazi ngumu kama vile za kulima ... Anasema tegemeo pekee la mama yake na huyo mtoto yatima kwa ajili ya mahitaji muhimu ni yeye .
25,000 YA TASAF YABADILI MAISHA YA JOYCE AJENGA NYUMBA, AENDA CHUO CHA UFUNDI.
Joyce anasema ilikuwa mwaka 2015 ndipo alipofikiwa na kuunganishwa kwenye Mpango wa kunusuru Kaya masikini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambapo baada ya kujiunga na Mpango huo maisha yake yalianza kubadilika.
Anasema kwa kuwa alikuwa amejifunza ujasiriamali kidogo pamoja na elimu ambayo wanapewa na viongozi wao wa TASAF ngazi ya Wilaya pindi wanapopokea ruzuku ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuhifadhi kidogo kidogo.
"Hela ya TASAF imenisaidia sana kwani nilitumia kwa ajili ya matumizi nyumbani lakini nyingine nilifanikiwa kuitunza baadae nikaweka vibarua wa kufyatua tofari nikazichoma na kujenga nyumba yangu ambayo ina chumba kimoja na sebule" anasema.
Anasema kabla ya fedha hizo za TASAF yeye alikuwa analala sebureni kwenye nyumba ya mama yake ... Jambo ambalo anadai kuwa lilikuwa linamkosesha amani.anasema yuko huru kwenye nyumba yake ambayo imekamilika kwa kusakafia chini kuweka mlango mzuri , ambayo ameanza kuishi mwaka 2021 japo bado madirisha hayajakamilika.
Anasema pia fedha Hiyo ya TASAF ilimsaidia kuongeza kipato kwa sababu alijiunga kwenye michezo ya kuchangishana (vikoba) Hivyo alipopokea fedha yake alinunua mbolea na kukodi mashamba ya kulima mahindi na karanga kwa ajili ya chakula nyumbani na mengine ya ziada kuuza.
AJIPELEKA CHUO CHA VETA
Anasema toka akiwa mdogo ndoto yake ilikuwa kuwa fundi mfumaji na mshonaji mkubwa, Hivyo alipomalizia kujenga nyumba yake aliamua kujipeleka chuo Cha VETA Cha Walemavu kilichopo Iyunga Mbeya kwa ajili ya kujifunza fani ya ufumaji na ushonaji.
"Kwa kweli nafurahi sana nimekutana na wenzangu , Lakini naona ndoto zangu zinakwenda kutimia za kuwa mfumaji na mshonaji mkubwa kwa Siku za mbeleni ,
Huu ni mwezi wangu wa nane toka nijiunge na chuo cha Veta , ada yetu ni shilingi 25,0000 ambayo namshukuru Mungu nalipia kidogo kidogo , muda mwingine nashindwa kulipia kwa wakati lakini huwa nawaomba walimu wangu wananielewa kuwa ntalipia miezi ya mbele nikipokea fedha ya TASAF na kuuza baadhi ya mazao " anasema Joyce .
Kwa miezi nane aliyosoma anasema tayari amejua kushona na kufuma vitambaa mbalimbali, japo changamoto kubwa ni mtaji wa kupata cherehani ambayo itamrahisishia kazi yake hiyo.
Joyce anatoa shukrani kwa TASAF kwa mchango wao uliofanikisha yeye kuhifadhi fedha kidogo kidogo na kufanikiwa kuanza mafunzo Veta . Anasema alikuwa analipwa shilingi 25,000 Lakini baada ya kujiunga na chuo wamemwongezea fedha ya ruzuku na kufikia shilingi 52,000.
AWAOMBA WADAU KUMSAIDIA BAISKELI YA KUTEMBELEA PAMOJA NA CHEREHANI.
Anasema anaiomba watanzania na mashirika mbalimbali kumsaidia Baiskeli ya kutembelea pamoja na cherehani kwa ajili ya kushonea nguo na vitambaa mbalimbali Ili aweze kujikwamua kiuchumi.
Anasema kipindi Cha mvua huwa anapata wakati mgumu hasa akiwa shambani ambapo muda mwingine mvua humnyeshea na kumwishia huko huku akipata wakati mgumu wa kutambaa kwenye tope wakati akirudi nyumbani.
NDOTO ZAKE NI KUSAIDIA WALEMAVU, WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM NA YATIMA
"Malengo yangu nikifanikiwa ni kuwasaidia walemavu wenzangu ,watoto wenye uhitaji maalumu na watoto yatimaa wanaopata shida mpaka hivi sasa kwa kukosa mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi na maradhi "anasema Joyce
Anasema anatamani awasaidie awape elimu bure ya ufundi na ujasiriamali Ili waweza kupiga hatua za kimaisha, anadai kuwa Kuna kundi kubwa la walemavu ambao wanapitia changamoto nyingi za maisha pasipo kupata Msaada wa Jamii zinazowazunguka.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Maji moto Ngalawa Mgogo anasema Joyce amekuwa mtu wa mfano kijijini hapo kwa bidii yake ya kazi na namna anavyotumia fursa ndogo ndogo akipata , alisema pamoja na ulemavu wake yeye ndie nguzo kubwa kwa mama yake kwa kumsaidia mahitaji muhimu kama chakula na maradhi.
“Kwakweli huyu dada huwa anatushangaza sana pamoja na ulemavu alionao huwa anatumia jembe dogo kulima , pia huwa anapanda na kupalilia karanga , ila kipindi cha mvua huwa anapata anakuwa na wakati mgumu sana namna ya kutembea kwenye tope kwa sababu hana vifaa muhimu vya kutumia mfano baiskel” anasema Mgogo
Naye mdogo wake Maiko Mwazembe ambaye ndiye humsaidia kumchukulia bidhaa mbalimbali za ujasiriamali anasema dada yake ambaye ni Joyce amekuwa msaada mkubwa kwa mama yao kwa hasa kipindi ambacho wao wameoa na kutokuwa karibu sana na mama yao kutokana na kuishi mbali pamoja na kutingwa na majukumu ya familia zao pia.
Mratibu wa TASAF Mbozi Agness Mwansembo anasema wakati Joyce ni mfano mzuri wa wanufaika ambaye fedha yake ambayo anaipata inabadilisha maisha yake kwa kasi kubwa tofauti na walengwa wengine licha ya ulemavu alionao.
Anasema pamoja na kuwafikia walengwa katika vijiji vyote 127 na Mitaa sita ndani ya Wilaya ya Mbozi , anasema kuwa wanawasimamia pia wanufaika walemavu kwa kuwaunganisha na ofisi ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa ajili ya walemavu
Comments