Daktari ajinyonga akijiandaa kutoa mahari
Muktasari:
Moyo wa mtu kichaka, ndivyo unavyoweza kusema unaposimuliwa tukio la Dk Joseph Ngonyani kudaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka akiwa nyumbani kwake kitongoji cha Saghana na kuacha simanzi na vilio kwa ndugu na majirani.
Moshi. Moyo wa mtu kichaka, ndivyo unavyoweza kusema unaposimuliwa tukio la Dk Joseph Ngonyani kudaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka akiwa nyumbani kwake kitongoji cha Saghana na kuacha simanzi na vilio kwa ndugu na majirani.
Ngonyani aliyekuwa mfanyakazi wa zahanati ya Saghana iliyopo nje kidogo ya mji wa Himo Kata ya Makuyuni wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kujinyonga Jumamosi Novemba 26, 2022, siku ambayo ilikuwa ni ya kupeleka mahari ukweni na ikiwa umebaki mwezi mmoja kabla ya siku ya harusi yake Desemba 28.
Inaelezwa kuwa muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea ukweni kutoa mahari, aliwaambia aliokuwa aambatane nao, watangulie na yeye angewafuata, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda na wao kukaribia ukweni, wakaanza kumpigia simu, ambayo iliita kwa muda bila majibu na baadaye ikawa haipatikani kabisa.
Akizungumza na Mwananchi jana, mhudumu wa usafi wa zahanati hiyo, Julitha Michael alisema siku ya tukio Dk Ngonyani alikuwa kazini hadi saa nane mchana akatoka na kuaga kuwa angerudi baada ya muda mfupi.
“Alirudishia milango akatuaga kuwa anatoka angerudi lakini hakurudi na tulipojaribu kumtafuta baadaye kujua nini kimetokea akawa hapatikani kwenye simu. Tulienda kuulizia anakoishi wakasema hawajamuona na wanachojua huwa analala hospitalini kwa sababu alikuwa mwenyewe kazini, mwezake ameondoka wiki mbili zilizopita hajarudi, hivyo tukafanya mawasiliano na ndugu zake ili kujua kama wamewasiliana na wanafahamu alipo, lakini nao hawafahamu.
“Jana Jumapili (juzi) saa 4:00 asubuhi, tukapata taarifa amejinyonga chumbani kwake, hajaacha ujumbe wowote. Alikuwa ni mtu wa watu na alikuwa na kawaida akitoka asubuhi lazima atuage,” alisimulia Julitha.
Alisema Dk Ngonyani alitarajia kuoa Desemba 28, mwaka huu na sherehe ingefanyikia nyumbani kwao Songea, Desemba 18 ilikuwa iwe ‘Send off’ ya mchumba wake ambayo ingefanyikia Lotima nchini Kenya.
Mshenga wa Dk Ngonyani, Alex Athuman Mzee alisema baada ya kufika nyumbani kwa msichana, walitakiwa kutoa ng’ombe 10 na mbuzi 20 ambayo ni sawa na Sh 4.6 milioni na kijana aliniambia yuko sawa hakuna shida
“Juzi Disemba 23 ndiyo tulikuwa tupeleke mahari, lakini kule kwa msichana kukawa na msiba nikamuelezea kijana akasema twende Jumamosi Novemba 26, na ilipofika siku hiyo saa mbili asubuhi tulionana akaniambia mzee tutaenda leo hakuna shida kila kitu kiko tayari. Saa nne nikamfuata kumwambia kuna kitu kinahitajika kitangulie, akanunua kikatangulia, saa saba nikamtafuta nikamwambia muda umeenda akaniambia kwa kuwa kuna kitu anasubiri, mimi na mama tuliokuwa tukienda tutangulie, atatufuata, lakini yule mama akasema tusubirie, Saa nane nikampigua simu akasema anakuja twende na saa tisa ilipofika akawa hapatikani hadi asubuhi kesho yake, naambiwa amefariki kwa kujinyonga”.
Mwananchi lilimtafuta kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanajro azungumzie tukio hilo, alijibu kuwa yuko kwenye ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani atafutwe baadaye.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Saghana, Kenedy Nangu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akieleza kuwa chanzo cha tukio hilo mpaka sasa hakijafahamika.
Comments