BABA PAROKO MAHAKAMANI KWA WIZI WA MILIONI ZA MGONJWA MAHUTUTI
Paroko wa Parokia ya Haydom Jimbo la Mbulu mkoani Manyara, Bartazari Margwe Sule (63) amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa akituhumiwa kuiba zaidi ya shilingi milioni 20 kwenye akaunti ya kaka yake Dionice Margwe Sule, ambaye inadaiwa kuwa ni mgonjwa wa kupoteza kumbukumbu, huku ikielezwa kwamba fedha hizo anazotuhumiwa kuziiba zimetokana na mirathi ya shemeji yake.
Kesi hiyo namba 44 ya mwaka 2022 iliyosomwa na Hakimu Mariam Luselwa inawakabili washtakiwa watatu, ambao ni Paroko Bartazari Sule, Cynthia Nyamtiga (27) pamoja na Winftida Rwakilomba (30) ambao ni watumishi wa benki ya NMB.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa Paroko Baltazari anakabililiwa na makosa mawili, ambapo la kwanza ni wizi, na pili ni kugushi.
Washtakiwa wengine Cynthia Nyamtiga na Winfrida Rwakilomba wote kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kushindwa kuzuia utendekaji wa kosa kinyume na kifungu 383 na kifungu cha 35 vya kanuni ya adhabu sura namba 16 kama ilivyofanyiwa marejeo 2022.
Washtakiwa hao watatu kwa pamoja wamekana kutenda mashtaka yanayowakabili, na wapo nje kwa sharti la kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshtakiwa pamoja na bondi ya milioni saba kwa kila mdhamini.
Shauri hilo limepangwa tena Disemba 21 mwaka huu kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.
Comments