TAKUKURU YAWAPANDISHA KIZIMBANI VIGOGO MUWASA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Katavi imewafikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA) Hussein Nyemba na Kaimu Ofisa Utumishi Justine Wambali, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Katavi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Katavi imewafikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA) Hussein Nyemba na Kaimu Ofisa Utumishi Justine Wambali, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Vigogo hao wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda leo Alhamisi Desemba 29, 2022 wakishtakiwa kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara taasisi hiyo zaidi ya Sh 17 milioni.
Imeelezwa, Novemba 1, 2022 wakiwa kazini kwa nia ovu, walitumia madaraka vibaya kuajiri ajira mpya 37 pasipo maelekezo ya bodi, kinyume na kifungu cha 12 kidogo cha (1)(b) na (e) cha sheria ya usambazi maji na usafi wa mazingira ya 2019.
Pia, watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa lengo la kujinufaisha wenyewe na kosa la pili ni kuisababishia hasara mamlaka ambapo katika tarehe tofauti Novemba 2022 wakiwa ofisi za MUWASA walishindwa kutumia vyeo vyao kwa weledi hivyo kusababisha hasara ya Sh17.81 milion.
Watuhumiwa hao baada ya kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Gosper Luoga wamekana kisha dhamana kuwekwa wazi ambapo Nyemba amekidhi vigezo na kuachiwa huru huku Wambali akirejeshwa rumande.
Hata hivyo, Hakimu Luoga kabla ya kuahirisha kesi hiyo amesema upelelezi umekamilika ambapo kesi hiyo itasikilizwa Januari 17, 2023.
Awali, Naibu Kamanda wa Takukuru mkoa wa Katavi, Stuart Mwamkaya akizungumza na wanahabari amesema wamechukua hatua hiyo kutokana na agizo la Waziri la Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa hivi karibuni akiwa ziarani mkoani humo kuwafanyia uchunguzi Mkurugenzi MUWASA na Afisa ardhi wilaya ya Tanganyika baada ya kubaini dosari.
“Huyu Wambali ametuhumiwa kwasababu alikuwa kaimu afisa utumishi kwa muda mrefu, alishindwa kumshauri mkurugenzi wake kuacha kuajiri zisizotambulika,” amesema
“Afisa Ardhi bado tunamfanyia uchunguzi upelelezi ukikamilika atachukuliwa hatua,” amesema Mwamkaya.
Comments