TAMISEMI YAPIGA "STOP" MWANAFUNZI WA KUTWA KUHAMIA BWENI
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amesema hakutakua na uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa kuhamia bweni.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amesema hakutakua na uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwenye shule za kutwa kuhamia bweni.
Taarifa iliyotolewa na Tamisemi imesema, Profesa Shemdoe ametoa agizo hilo jana Alhamisi Desemba 29, 2022 Dodoma katika kikao kazi cha kufanya tathmini ya usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini kwa mwaka 2022 kwa maofisa elimu wa mikoa.
Profesa Shemdoe alisema tangu Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki atoe taarifa ya kuwapangia shule wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023, Desemba 14, 2022, Wizara hiyo imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wazazi ama walezi ya kuomba watoto wao kuhamia kwenye shule za bweni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ugonjwa au matamanio ya wazazi au watoto.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Shemdoe alisema hakutakuwa na uhamisho wa wanafunzi waliochaguliwa shule za kutwa kwenda kwenye shule za bweni kwani upangaji wa wanafunzi umefuata vigezo na taratibu zilizowekwa.
"OR-Tamisemi inasisitiza hakuna uhamisho kutoka shule ya kutwa kwenda bweni kwasababu wale waliopangiwa bweni wamekidhi vigezo vya kuchaguliwa katika shule hizo," alisema
"Na kwa wanafunzi wenye changamoto za kimazingira, mfano amehama makazi ya awali wawasilishe changamoto hizo kwa Makatibu Tawala wa Mkoa ili zitatuliwe, maana upangaji wa wanafunzi kwenye shule umezingatia ukaribu wa shule na makazi ya wanafunzi hivyo endapo wamehama makazi ya awali kunaweza kutokea changamoto ya umbali," alisema Profesa Shemdoe.
Prof Shemdoe alisema kupangiwa shule kwa wanafunzi kumezingatia viwango vya ufaulu, ushindani pamoja ukaribu wa shule na makazi.
Aidha, idadi ya wanafunzi waliopangiwa kwenye shule za bweni imezingatia viwango vya juu vya ufaulu na nafasi zilizokuwepo katika shule hizo ili kuepusha msongamano kwa wanafunzi darasani na mahali pakulala.
Endapo zitatokea nafasi za bweni zitakazohitajika kujazwa hapo baadae, maombi yatakayokuwa yamefikishwa Ofisi ya Rais-Tamisemi makao makuu yatachambuliwa na kamati maalum ambayo itaangalia sifa za walioomba kuhamishiwa huko.
Prof Shemdoe alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kwa wakati na kwamba hakutakua na chaguo la pili la mwanafunzi.
"Kwa mwaka huu hakutakuwa na chaguo la pili la wanafunzi kwasababu fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya elimu zimetosha kuboresha miundombinu ya kuwachukua watoto wetu wote kwa intake (mkupuo) mmoja."
"Tangu Rais aingie madarakani ameshatoa fedha zilizowezesha kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa 20,000 nani ya miaka miwili hatua ambayo imewaondolea adha watoto kwa kuanza masono kwa pamoja huku wazazi wakiwa hawajachangishwa kitu."
Comments