WAZIRI MKUU ATAKA WATUMISHI KUTENGA SIKU TATU ZA KWENDA VIJIJI I KUSIKILIZAKERO ZA WANANCHI
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi kwenye Halmashauri zote nchini kutenga siku tatu kati ya siku za kazi kwenda vijijini ili kutatua changamoto za wananchi.
Amesema kuwa ni lazima watumishi wa umma wajue wajibu wao mkubwa ni kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Desemba 16, 2022 wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa umma wa Halmashauri za mkoa Rukwa ambako alikuwa kwenye ziara ya kikazi.
Amesisitiza kuwa, “Hawa wananchi wamesambaa katika Wilaya na halmashauri, tumejenga majengo ya ofisi sio lazima wananchi waje humo kupata huduma, wapo wengine hawawezi kuja hapa lakini wanahitaji Serikali yao inahudumi.”
Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amewataka viongozi katika halmashauri kuhakikisha wanasimamia watumishi kutokaa ofisini wiki nzima badala yake waende vijijini kwani huko ndiko wananchi walipo ili wawasikilize na kuwatumikia.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amewataka watumishi wanaosimamia eneo hilo kufanya makadirio yenye uhalisia na kutambua vyanzo vyote ambavyo vinaweza kuingiza mapato “lazima mfanye tathmini eneo fulani linaweza kuwaingizia kiasi gani, kwa siku, kwa mwezi au kwa mwaka.
“Tunapotaka kukusanya mapato ya ndani anzeni kwa kubaini vyanzo na msiwaachie wakuu wa idara pekee. Mameya na wenyeviti wa halmahauri tushiriki kikamilifu, watendaji wa vijiji na kata hata watumishi wengine, tukishabaini turudi kusimamia sote,” amesema.
Awali akikagua kituo kikuu cha mabasi Sumbawanga kilichopo eneo la Katumba, Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Jacob Mtalitinya kukutana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ili kuweka utaratibu wa kituo hicho kilichogharimu Sh7.9 bilioni kianze kutumika.
Majaliwa ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege cha Sumbawanga “Viwanja vitatu vya Mara (Musoma mjini), Shinyanga na hapa Sumbawanga vipo kwenye mpango wa kujengwa, kile cha Lindi kitajengwa na mradi wa gesi, Rais wetu anajua matakwa ya watanzania,” amesema.
Jana wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga kilichopo katika kijiji cha Pito, Majaliwa aliagiza kuwa ujenzi wa vyuo vya Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) nchini usimamiwe na makatibu tawala wa mikoa badala ya kusimamiwa na mamlaka hiyo makao makuu.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha vyuo hivyo kuwa na usimamizi wa karibu hivyo kukamilika kwa wakati na viwango stahili.
“Narudia tena, VETA wabadilishe mifumo yao ya ujenzi vyuo na visimamiwe na Makatibu Tawala wa mikoa na kama kuna mtumishi wa VETA ataletwa atakuwa chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa mkoa ili uratibu uwe jirani zaidi,” amesema.
Comments