ASILIMIA 63 YA WANAFUNZI SONGWE HAWAJARIPOTI MASHULENI

 Zaidi ya wanafunzi 13,000 sawa na asilimia 63 wa kidato cha kwanza mkoani Songwe waliochaguliwa kuanza masomo Januari 9 mwaka huu, hawajaripoti shuleni hadi leo Ijumaa.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda amesema hayo leo wakati akitoa salamu za mkoa katika kikao kazi cha wasimamizi wa elimu katika shule za msingi na sekondari mkoani hapa kuwa kunahitajika jitihada ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza waanze pasipo kuwa na visingizio.

Amesema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ni kuwa ni 22,986 lakini hadi Januari 11 wanafunzi 7,772 ndiyo walioripoti, amewataka wazazi kuwapeleka wanafunzi hao shule bila kujali kama wana sare au hawana.

Pia, Seneda amewataka walimu na viongozi wa elimu kuhakikisha wanatatua haraka changamoto za walimu na kuwapa mrejesho ili kutoa nafasi waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo.

"Uandikishwaji wa darasa la awali hadi jana (Alhamisi) ni watoto 23,860 kati ya wanafunzi 33,815 waliokusudiwa, na uandikishwaji wanafunzi darasa la kwanza ni 30,268 kati ya waliokadiriwa 37,671," amesema Seneda.

Naye Mkurugenzi wa elimu na Utawala Ofisi ya Rais Tamisemi, Vincent Kayombo amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na maofisa elimu kuhakikisha kila kiongozi anasimamia aliyeko chini yake katika idara ya elimu ili kusimamia ipasavyo majukumu ya kuendeleza mafanikio katika elimu.

"Zipo changamoto za baadhi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kutokujua kusoma kuandika na kuhesabu (KKK), kwa darasa la saba mwanafuzi kumaliza bila kujua kuzungumza lugha ya Kiingereza na kidato cha nne wanaopata daraja la 1 na 2 kuwa wachache," amesema Kayombo.

Sanjari na hayo Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Cosmans Nshenye akisoma hotuba ya Naibu Waziri wa Tamisemi, David Silinde amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kiasi cha Sh29 bilioni kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji wa elimu bila ada hivyo wazazi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuchangia chakula kwa kila mtoto kupata mlo wa mchana shuleni ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kuondokana na udumavu kwa watoto.

Mwalimu Maiko Nzunda amesema wao wamekuja kusikiliza maelekezo wanayopewa na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE