KAMPUNI ZA SIMU ZAWAKANA WALIOPANDISHA VOCHA ZA SIMU
Siku chache tangu Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania, TCRA-CCC kukemea baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya vocha, Umoja wa Kampuni za Simu Tanzania (TAMNOA) umewataka wananchi kutonunua vocha kwa bei ya juu zaidi ya iliyochapishwa.
Dar es Salaam. Siku chache tangu Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania, TCRA-CCC kukemea baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya vocha, Umoja wa Kampuni za Simu Tanzania (TAMNOA) umewataka wananchi kutonunua vocha kwa bei ya juu zaidi ya iliyochapishwa.
Januari 10, 2023, TCRA-CCC ilisema mtu yeyote anayeuza vocha kwa bei tofauti na iliyoidhinishwa anafanya kosa la jinai.
Kauli hiyo imekuja baada ya malalamiko ya wananchi kupanda kwa vocha kutoka Sh500 hadi Sh550 au Sh600 wakati iliyokuwa ikiuzwa Sh1, 000 ikiuzwa kwa Sh 1,100 katika maeneo mbalimbali Tanzania.
Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana Jumatano Januari 11, 2023 na kusainiwa na Mwenyekiti wa TAMNOA, Philip Besimire ilieleza kuwa kampuni za simu nchini hazijafanya mabadiliko yeyote kwenye bei za vocha hizo.
“Imebainika kuwa mabadiliko hayo yanafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanatoza bei kubwa kuliko iliyopangwa na kuchapisha kwenye vocha husika, kitendo hiki ni kinyume na utaratibu tuliokubaliana nao na tunakemea vikali,”inaeleza taarifa hiyo.
TAMNOA imewaasa wananchi kutonunua vocha kwa bei ya juu zaidi ya ile iliyochapishwa kwenye vocha na endapo watauziwa vocha kwa bei tofauti wawaripoti wauzaji kwenye vituo vya huduma kwa wateja vya mitandao hiyo.
Pia umoja huo umewakumbusha wananchi kununua vocha kupitia maduka ya mawakala pamoja na huduma za kidigitali.
Comments