HAKIMU AUWAWA KWA KIPIGO CHA WANANCHI RUNGWE
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Dk Vicent Anney amesema watu wawili wameuawa akiwemo hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Handeni, Joachim Mwakyoma baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira.
Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Dk Vicent Anney amesema watu wawili wameuawa akiwemo hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Handeni, Joachim Mwakyoma baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Januari 22, 2023, Dk Anney amesema tukio hilo limetolea katika kijiji cha kibole halmashauri ya Busokelo.
Amesema hakimu huyo alikuwa ameambatana na wenzake wawili kwenda kwenye shamba lenye mgogoro na wanakijiji walishinda kesi katika Mahakamani Kuu Desemba mwaka 2022 baada ya kesi hiyo kusikilizwa mahakamani kwa miaka zaidi ya 10.
Dk Anney amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa kitendo cha hakimu na wenzake kuingia katika shamba hilo kiliwashtua wananchi waliowafuata na kuwahoji na yakaibuka malumbano.
Amesema katika tukio hilo wananchi wawili walipigwa risasi na mmoja wa watu waliokuwa wameambata na hakimu na walikimbizwa katika hosptali ya Itete kwa matibabu zaidi na hali zao zinaendelea vizuri .
Dk Anney marehemu licha ya kuja kijiji hapo kwa ajili ya mapumziko, pia alikuwa kwenye taratibu za kukata rufaa mahakamani kupinga hukumu.
“Kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo kuwasaka watu waliohusika na mauaji. Wilaya hii imekithiri matukio ya mauaji yanayohusiana na migogoro ya ardhi, ”amesema.
Akigusia tabia isiyofaa ya wananchi kujichukulia sheria mkononi Dk Anney amesema, "tunaendelea kushughulikia matukio hayo ikiwepo kushirikisha na viongozi wa dini, kamati za amani wilaya kuona wanakemea na kutoa elimu kwa jamii kuachana na tabia ya kuchukia sheria mkononi."
Diwani wa Busokelo ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri, Anyosisye Njobelo amesema, "ndio tukio hilo limetokea kwenye kijiji kilicho katika kata yangu ila kwa sasa mimi sio mzungumzaji tuviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake."
Mmoja wa wananchi wa kata ya Kiwila Wilaya ya Rungwe ambaye aliomba jina lake lisitajwe amesema changamoto kubwa ni mienendo ya kesi za migogoro ya ardhi zinavyoendeshwa kwenye vyombo vya maamuzi .
“Tukisema kwa Tanzania, Rungwe kuna migogoro mingi sana ya ardhi, mauaji lakini tushukuru Mungu ujio wa Mkuu huyu wa Wilaya, Dk Vincent Anney ameweza kudhibiti kwa wananchi wanaohusika kukamatwa na kuchukuliwa hatua kidogo imesaidia,” amesema.
Comments