MUUAJI WA MFANYAKAZI WA TANESCO SONGWE NAE AUWAWA
Polisi Mkoa wa Songwe imesema mtu anayedaiwa kumuua kikatili mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Angela Shekinyau (33) usiku wa kuamkia Jumatatu ya wiki hii naye ameuawa wakati akijaribu kukimbia akiwa chini ya ulinzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 18, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa Theopista Mallya amesema polisi walimkamata mtuhumiwa Isaya Juma Mazuge maarufu kwa jina la ‘Wa Uyole’.Kamanda huyo amesema baada ya kukamatwa alitoa ushirikiano kwa kuonyesha vitu vya marehemu Agela ikiwamo simu ya Iphone 11PRO MAX na kuwataja wenzake.
Ameendelea kusema kuwa, mtuhumiwa huyo pia alikuwa na Bastola iliyotengenezwa kienyeji na kwamba waliikuta ikiwa na ganda la shotgun pamoja na mapanga.
Amesema mtuhumiwa alikuwa ameficha silaha hizo kwenye Msitu wa Vwawa Day na baada ya kuonyesha ushirikiano aligeuka ghafla na kuanza kukimbia jambo lililowafanya polisi warushe risasi mbili juu na moja ilifyatuliwa kwake na hatimaye kumpiga na kusababisha kifo.
Kamanda amesema kijana huyo alifariki dunia baada ya damu nyingi kuvuja akipelekwa hospitalini.
Amesema wanaendelea kuwasaka waliotajwa ili wafikishwe mahakamani.
Tukio la kuawa kwa mfanyakazi wa Tanesco limewashtua wakazi wengi wa mkoa huo akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Waziri Kindamba ambaye aliwaagiza polisi wawasake wahusika kwa udi na uvumba
Comments