WATOTO WATATU FAMILIA MOJA WATEKETEA KWA MOTO
Watoto watatu familia moja walivyoteketea kwa moto Rombo
Eneo la sehemu ya nyumba iliyoungua na kuteketeza watoto watatu wa kiume katika kijiji cha Lessoroma, wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Rombo. Ni tukio linaloweza kudumu katika kumbukumbu ya maisha ya Karesma Theodory (39) wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kushuhudia watoto wake watatu wakiteketea kwa moto.
“Nilisikia watoto wakiniita, mama mama huku moto ukiwa umeshika kasi,” alisimulia Karesma ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Lessoroma wilayani Rombo na kueleza namna alivyojitoa mhanga kuwaokoa wanawe pasipo mafanikio.
Tukio hilo lililoibua simanzi, lilitokea usiku wa kuamkia juzi kijijini humo kwa kile kinachodaiwa chanzo ni kibatari ambacho watoto walikuwa wakikichezea ndani ya nyumba yao.
Watoto hao waliofariki dunia kwa kuteketea kwa moto wakati mama yao akiwa ametoka nje akiongea na simu na mume anayeishi nchini Kenya ni Erick (9), Joshua (7) na Gidion Theodory (2).
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo cha moto ni kibatari ambacho watoto hao walikuwa wakikichezea ndani wakati mama yao akiwa nje.
“Ni kweli hili tukio limetokea jana (juzi) usiku, lakini chanzo chake ni kibatari walichokuwa wakikichezea hawa watoto, mama yao akiwa hayupo, kwa hiyo hiki kibatari kilidondoka kisha nyumba kushika moto,” alisema Kanali Maiga.
Mtendaji wa Kijiji cha Lessoroma, Emma Mosha alisema tukio hilo limewashtua na kuwashangaza wengi na kusema kuondokewa na watoto watatu wote kwa mpigo sio jambo jepesi.
“Kwa kweli hili tukio limeniumiza sana, ni tukio gumu, yaani halivumiliki, kuondokewa na watoto watatu na wamekufa kifo cha mateso sio kitu cha kawaida, kwa kweli limetuumiza sana,” alisema Emma.
Mmoja wa majirani, Atanasi Joseph, alisema: “Yaani kwa kweli hatujui tuseme nini, maana hili tukio ni gumu, kuondokewa na watoto kwa wakati mmoja ni pagumu kidogo, cha msingi tunamwombea huyu mama uvumilivu maana sio kitu rahisi.”
Miili ya watoto hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Kituo cha Afya cha Karume kilichopo wilayani humo kwa ajili ya taratibu za maziko.
Mama asimulia
Akielezea tukio hilo lilivyotokea, Karesma alisema alitoka nje na kuwaacha watoto wake hao wakiwa chumbani na yeye akaenda kuongea na simu na mume wake anayeishi Kenya.
Alisema wakati amesimama alisikia sauti ya watoto ikiita, “mama mama,” alipogeuka aliona moto unawaka kwenye nyumba yake na kurudi mbio ili kwenda kuwaokoa watoto waliokuwepo ndani.
“Nilikuwa nimetoka nje kuongea na simu ya wifi yangu, nikawa nimesogea hadi kichumini. Nilikuwa nimewaacha watoto wangu ndani, wakati nasema nimpe wifi yangu simu yake nikasikia kelele,” alisema.
Karesma alisema moto huo ulikuwa unawaka sebuleni huku watoto wakiwa chumbani, alipambana kuwaokoa kwa kuvunja mlango wa chumbani lakini alishindwa baada ya moto kumpiga machoni na sehemu ya mkononi.
“Nilijaribu kuvunja chumba walichokuwa wanangu nikashindwa maana niliishiwa nguvu, nilishindwa kupiga hata ukunga kutokana na zile sauti za wanangu,” alisema.
Mwanasaikolojia Josephine Tesha wa jijini Dar es Salaam alisema mtu anapopatwa na tukio la aina hiyo anatakiwa aachwe aomboleze kwa hali yake ya asili bila kuzuiwa ili yale machungu yaondoke, kumzuia inaweza kumletea madhara.
“Huyu mama amepitia kipindi kigumu sana kwa tukio lilivyo. Mtu wa aina hii unatakiwa umpe hadi miezi sita ili amalize ule uchungu kiasili kabisa usimzuie. Baada ya huo muda ni vizuri akaonana na mwanasaikolojia.”
Alisema kama asipopatiwa ushauri nasaha uchungu unaweza kumsumbua kipindi kirefu cha maisha yake na hili linazuilika tu kwa kumuwahi na kumpatia ushauri nasaha.
Comments