MKUU WA POLISI(OCD),OFISA UPELELEZI (OC CID)WASIMAMISHWA KAZI KWA UNYANYASAJI
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amewasimamisha kazi Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kilombero baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa wanawanyanyasa.
Kilombero. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amewasimamisha kazi Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), SSP Shedrack Kigomanya na Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kilombero, SP Daud Mshana baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa wanawanyanyasa.
Masauni amechukua hatua hiyo jana Jumatatu, Februari 20, 2023 akiwa kwenye ziara wilayani Kilosa ambapo pamoja na kukagua baadhi vituo vya polisi na magereza yaliyopo pia alizungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Waziri Masauni pia amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura kuwachunguza na kuwahamisha viongozi hao ili kujenga imani kwa wananchi na pia kuimarisha dhana ya uwajibikaji.
Vile vile amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama kuwahamisha askari wote wanaotajwa kunyanyasa wananchi na kuleta askari wapya na kuhakikisha anaweka wengine kwenye kila kata ili kusogeza huduma ya kiusalama karibu na wananchi.
"RPC nakuagiza hebu chukua hatua na ikiwezekana safisha askari wote wanaoonekana kwenda kinyume na sheria na miongozo ya jeshi la polisi,
“Serikali hatuko tayari kuona askari wachache wasiokuwa waadilifu wanalichafua jeshi letu, tuko kwenye kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye tayari alishasema kuwa hataki kuona mwananchi ananyanyaswa ma askari ama kiongozi yeyote eti kwa sababu ya cheo, fedha ama dhamana aliyonayo," amesema Mhandisi Masauni.
Hata hivyo aliwataka wananchi kujenga imani na jeshi la polisi na kufuata sheria za nchi ikiwa ni pomajo na kuheshimu mamlaka zilizowekwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Danstan Kyobya amesema kuwa wilaya hiyo kwa kiasi kikubwa iko salama licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo ikiwemo ya wananchi wengi kukosa namba na vitambulisho vya Taifa hali inayosababisha baadhi yao kushindwa ama kuchelewa kupata huduma za msingi.
Kufuatia changamoto hiyo mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa bado inaendelea kushughulikiwa kwa kwa kuwahusisha mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Awali wakieleza changamoto wanazokutana, baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Ifakara wamedai wamekuwa wakikamatwa bila ya utaratibu na kutozwa faini.
Mmoja wa waendesha bajaji, Boniface Ganga amesema kuwa askari wa usalama barabarani katika mji huo wamekuwa wakiweka vituo vya ukaguzi vingi na hivyo kusababisha usumbufu.
"Vijana wengi wa hapa Ifakara tumekataa kukaa vijiweni na kuacha kufanya vitendo vya uhalifu tumeamua kujiajiri kwenye bajaji na bodaboda, lakini hawa wenzetu askari wa usalama barabarani wamekuwa ni kero kila mahali wanaweka vizuizi kwa ajili ya ukaguzi, hii kwetu ni kero kubwa," amesema Ganga.
Naye Matha Mburuma mkazi wa Ifakara amedai kuwa baadhi ya polisi wamekuwa wakitumiwa na watu wenye uwezo wa kifedha wanaojiita wawekezaji kwa kuwapiga wananchi wanaokwenda kulima kwenye mashamba yao na kuwakamata na kuwabambikizia kesi za jinai.
Martha amedai kuwa mwishoni mwa mwaka jana yeye na wakulima wenzake wakiwa shambani walikuja askari Polisi wenye silaha za moto na kuwaamuru watoke shambani humo kwa kudai shamba hilo' ni mwekezaji na walipokaidi walitolewa kwa nguvu na kupelekwa kituo cha polisi na kufunguliwa kesi ya jinai ambapo mpaka sasa kesi hiyo haijafikishwa mahakamani.
Comments