POLISI ATEKWA APORWA SILAHA
Polisi mjini Narok wanawasaka watu wawili waliokuwa na silaha wanaoripotiwa kumteka nyara Fredrick Shiundu, Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Narok ya Kati Jumanne usiku kisha kumtupa karibu na mto.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Narok Kizito Mutoro amesema watu hao waliokuwa wamejihami na silaha walikuwa wakimvizia Shiundu nje ya nyumba yake na kumvamia alipofungua mlango wa nyumba yake.
“Watu hao walimpokonya silaha Shiundu kabla ya kumfunga kwenye gari aina ya Toyota Wish na kuendesha umbali wa kilomita 17 hadi eneo la Tipis ambako walimpora bastola yake aina ya Jericho ikiwa na risasi 14 kisha kumtelekeza afisa mkuu huyo wa polisi," amesema Mutoro.
Kwa mujibu wa kituo cha Televisheni cha NTV Kenya kimeripoti kuwa, Shiundu aliokolewa na maofisa wenzake siku ya Jumatano asubuhi, ambapo walifuatilia simu yake kwa njia ya mtandao baada ya mkewe kutoa taarifa.
Kulingana na Muturo, ambaye anasema yeye binafsi alimhoji Shiundu baada ya tukio hilo, washukiwa hao wangeweza kumpiga risasi OCPD lakini aliweza kuzungumza nao ili wasifanye hivyo.
Mutoro aliongeza kuwa polisi wameanza uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku akiwataka wananchi walio na taarifa zozote kuhusu kisa hicho kuripoti kwa polisi.
"Watu hawa wanaonekana kumfahamu na walikuwa wamemfuatilia. Bado hatujabaini sababu hasa za tukio hilo lakini tunashuku walikuwa wakiifuata bastola yake," amesema.
Comments