RC KINDAMBA " WAKANDARASI WABABAISHAJI KUCHUKULIWA HATUA
Songwe. Jumla ya mikataba 10 ya miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh14.27 bilioni imesainiwa na kuleta tumaini jipya kwa wananchi la kuondokana na uhaba wa maji.
Hafla ya utilianaji mikataba hiyo imefanyika leo Ijumaa February 17, 2023 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe na kushuhudiwa na Mkuu wa mkoa huo, Waziri Kindamba aliyewaonya makandarasi wababaishaji.
Kindamba amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwenye miradi inayogusa maisha ya kila siku ya watu ili kuona wanaondoka pale walipokuwepo katika shida ya kusaka maji na kuacha kazi ya uzalishaji ili shida hiyo imalizike na watu waendelee kufanya kazi ya Kujenga nchi.
"Leo mnaposaini mikataba mnatuonesha sura za upole, lakini mkienda kufanyakazi mnabadilika na kuanza kumsumbua, sasa nawaambia kama kuna mkandarasi aliyefika hapa kiujanjaujanja hana uwezo wa kufanya kazi namtaka aondoke vinginevyo hatabaki salama," amesema Kindamba.
Aidha Kindamba amemwagiza Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) kuchukua hatua kali kwa makandarasi wawili wanaotejeleza miradi ya maji Itumba - Isongole na ule wa Isansa ikiwemo kuvunja mkataba na kuzuia malipo yao.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Mkoa Songwe Mhandisi, Charles Pande amesema wamejipanga kusimamia miradi hiyo na kufuta kabisa kuwa na miradi kichefuchefu.
Mwakilishi wa Mkandarasi hao, Athuman Mdee amesema makandarasi wamesikia maelekezo ya Serikali na kwamba watajitahidi kitekeleza kwani wanatambua malengo ya Serikali ni kuondoka changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema makandarasi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kucheleweshewa malipo ambayo ni chanzo cha kuchelewesha miradi.
"Baadhi ya miradi ya Serikali tumekuwa tukikabiliana na changamoto ya ucheleweshewa malipo, ambayo yanakwamisha kazi zetu na hata tukikopa benki lakini malipo kuchelewa yanatukwamisha sana," amesema Mdee.
Comments