MBUNGE MWENISONGOLE,WATUMISHI TANROADS NA WADAU WENGINE WAMWAGA VIFAA KWA WANAFUNZI WALIOANZA SHULE BILA VIFAA
Wadau mbalimbali mkoani Songwe wameombwa kujitokeza kusaidia michango na vifaa ili kuwawezesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ambao hawana vifaa na sare katika mkoa huo.
Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi Februari 18, 2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe (RAS), Happiness Seneda wakati wa mazoezi ya kujenga afya maarufu 'Back to School Songwe Jogging Club' yenye lengo la kuhamasisha wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni kujiunga na masomo.
Katika mazoezi hayo ambayo yameongozwa Katibu Tawala huyo wa mkoa yaliambatana na kukabidhi vifaa baadhi ya wanafunzi ambavyo vimetolewa na wadau mbalimbali.
Katibu Tawala huyo amesema kuwa vifaa hivyo vimechangiwa na wadau wakiwemo Tanroads ambao wamechangia vifaa vyenye thamani ya Sh300,000, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, George Mwenisongole akichangia vifaa vyenye thamani ya Sh50,000 huku Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC) likichangia madaftari kwa wanafunzi 17 huku akitoa rai kwa wadau wengine kuchangia.
RAS huyo ambaye ni mhamasishaji mkuu na mshiriki wa mazoezi hayo ya kujenga afya ya mwili amesema kuwa michango inayotolewa inasaidia wanafunzi amabo wameripoti shuleni bila vifaa.
"Nawaomba wadau kutoa michango mbalimbali ya vifaa vya shule ili tuwasaidie watoto wetu waende shule" amesema RAS Seneda
Pia, amewashukuru waliojitokeza kushiriki kwenye jogging hiyo akisema kuwa Jumamosi ijayo itakuwa wilayani Songwe.
"Mazoezi ni afya hatutaki vitambi fanya mazoezi kila siku ila Jumamosi ni ujuzi tu kuoneshana, Tunawashukuru sana waliochangia vifaa" amesema na kuongeza
"Mazoezi tunayoyafanya yana impact, kidato cha kwanza asilimia zimefika 86 na awali asilimia 97 tunafanya kampeni hii ili asilimia hiyo iliyobaki iende shule"
Amesema kuwa programu hiyo ambayo inakwenda kwenye wilaya zote za Mkoa wa Songwe ilianzishwa ili kuwahamasisha watoto ambao hawajajiunga na shule wajiunge hata kama hawana vifaa wala sare ambapo anatapokelewa aendelee na masomo huku wadau wanamchangia akiwa shuleni.
"Wiki ijayo tutakuwa Chitete Momba" amesisitiza Katibu Tawala hiyo wa Mkoa wa Songwe.
Nae Kaimu Meneja wa Tanroads Injinia Suleiman Bishanga amesema kuwa Tanroads ni sehemu ya jamii hivyo kwa kuthamini tukio hilo walihamasishana kuchangia Vifaa hivyo katika ofisi yao na wataendelea kuunga Mkono matukio yote ya kijamii ndani ya Mkoa wa songwe
Wanafunzi waliopewa vifaa ni pamoja na Jestina Manipembe wa shule ya Sekondari Nkanga, Flora Kashililika shule ya Shaji, Lena Ndidi wa Hezya Sekondari na Enelisa Mgala kutoka shule ya Sekondari Bara.
Jumla ya Wanafunzi wahitaji ni 300 kimkoa lakini wanaopata kimkoa 50 huku kwa wilaya ya Mbozi vifaa vimetolewa kwa wanafunzi 10.
Jogging hiyo ambayo hufanyika kila Jumamosi ni moja ya mkakati wa mkoa wa Songwe wenye lengo la kuwahamasisha wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza ambao hawajajiunga na masomo waripoti shuleni hata kama hawana vifaa na sare.
Comments