TUNDUMA:STOO YA KUHIFADHI VIFAA VYA UJENZI YAJENGWA KWA SHILINGI MILIONI 25
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mkoani Songwe limetoa siku 5 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Philemon Magesa kuhakikisha kuwa anawasilisha kwenye kamati ya fedha, taarifa ya matumizi ya shilingi milioni 383 za mradi wa ujenzi wa uzio wa soko la wamachinga
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Madiwani katika baraza hilo kutoridhishwa na taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, ikiwemo kibanda cha kuhifadhi vifaa vya ujenzi (Stoo) katika mradi huo kudaiwa kuwa ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi milioni 25.
Mbali na kuhoji gharama za ujenzi wa stoo, Madiwani hao wamelalamikia kitendo cha Mkurugenzi huyo kukaidi agizo la kamati ya fedha ya kupeleka vifaa vyote vya ujenzi kupelekwa eneo la mradi ikiwemo mifuko 1870 ya saruji, pamoja na kubadilishwa kwa ramani ya soko hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana kwenye kikao cha baraza kilichoketi kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa za robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/23 na kufanyika katika Ukumbi wa ofisi za Halmashauri zilizopo katika Mji wa Tunduma, Wilayani Momba.
Akifunga kikao cha Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayoub Mlimba, alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Magesa ambapo katika kikao hicho alimkaimisha, ofisa Maendeleo ya Jamii,
Mwanaisham Shemagembe,kuhakikisha ndani ya siku 5 awe amewasilisha taarifa yenye uchanganuzi wa matumizi ya fedha katika mradi huo wa soko la wamachinga linalojengwa kwa mapato ya fedha za ndani.
“Pamoja na kwamba mmetuambia kuwa mkaguzi wa ndani na kamati ya ulinzi na usalama imefanya ukaguzi kwenye mradi huo, Mkurugenzi nakuagiza ndani ya siku tano uwe umeeanda taarifa na kuiwasilisha kwenye kamati ya fedha”.
Alisema kamati hiyo ya fedha inatarajia kuketi Februari 6,2023 ambapo pamoja na mambo mengine inatarajia kwenda kufanya ukaguzi katika mradi huo wa soko.
“Mbali na kutuletea taarifa hiyo, pia tunataka uwaandalie usafiri wajumbe wa kamati ya fedha ili wafike kwenye mradi na kufanya ukaguzi” alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Halmashauri Mlimba.
Awali akichangia kwenye taarifa ya kamati ya fedha iliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, kwa niaba ya Mwenyekiti, Diwani wa viti maalum, Victoria Myombe, alitaka ufafanuzi juu ya mambo kadhaa juu ya mradi huo wa ujenzi wa soko la Wamachinga linalojengwa katika kata ya Majengo katika katika Halmashauri hiyo.
Miongoni mwa mambo hayo ni juu ya shilingi milioni 25 zilizotumika kama gharama za ujenzi wa stoo ya kuhifadhia vifaa vya ujenzi katika mradi huo wa soko la Machinga.
Kadhalika, alihoji juu ya ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kushindwa kutekeleza agizo la kamati ya fedha la kutaka vifaa vyote vya ujenzi katika soko hilo, ikiwemo mifuko 1870 ya saruji kushindwa kupelekwe na kuhifadhiwa kwenye eneo la mradi.
Akijibu hoja hizo, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ya fedha Frank Mponzi ambaye ni diwani wa kata ya Majengo, alisema ofisi hiyo ya Mkurugenzi licha ya kuagizwa mara kadhaa imeshindwa kutekeleza maagizo ya madiwani.
“Kuhusu hili la mifuko ya saruji kamati ya fedha ya fedha ilitaka iwe imefikishwa saiti tangu jumamosi (Januari 30,2023) lakini hadi leo hakuna kilichofanyika” alisema Diwani Mponzi.
Pia Mponzi alisema mbali na kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko hilo, aliwatuhumu watendaji hao kubadilisha ramani ya ujenzi wa soko hilo.
Hata hivyo, mwanzoni kikao hicho kilianza kwa mzozo baada ya Madiwani hao hoji sababu za Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Magesa kushindwa kushiriki kwenye kikao hicho na vingine vya Madiwani na badala yake hukaimisha.
Akitolea ufafanuzi kuhusu suala hilo la Mkurugenzi kukimbia vikao, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mulimba alisema kuwa mkurugenzi huyo yupo Dodoma kwenye vikao kwa ruhusa ya Katibu Tawala wa Wilaya (Das), pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa (Ras).


Maoni