WAKUU WA IDARA SIMAMIENI MIRADI-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini wasimamie kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao na wahakikishe inakamilika kwa wakati ili itae huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
“Huduma za jamii ndizo zinazogusa maisha ya kila siku ya wananachi kama elimu, maji, nishati, afya na kilimo, hivyo halmashauri zetu lazima ziongeze nguvu katika maeneo hayo. Wakuu wa Idara tumieni muda mwingi kwenda kwenye maeneo ambayo miradi inatekelezwa badala ya kukaa ofisini tu.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 15, 2023) wakati akizungumza na watumishi wa mkoa wa Songwe akiwa kwenye majumuisho ya ziara ya kikazi mkoani Songwe ya kukagua miradi ya maendeleo na mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapata katika kipindi cha miaka miwili.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji Tunduma kwa kujenga baadhi ya miradi kwa kutumia makusanyo ya ndani ukiwemo ujenzi wa madarasa 10 katika shule ya msingi Haisoja kwa gharama ya shilingi milioni 800, amewataka viongozi wa halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo.
“Viongozi wa halmashauri muwe wabunifu na mtumie fursa mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yenu ili ziwasaidie katika kuongeza mapato. “Shirikisheni na sekta binafsi hawa watawasaidia kuleta maendeleo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha mwelekeo kwenye hili. Tambueni mchango wao, lengo la Serikali ni kuendelea kufanya kazi na sekta binafsi.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewaelekeza viongozi wa wilaya, halmashari na wawakilishi wa wananchi waimarishe ushirikiano baina yao na watumishi wengine katika maeneo yao ili kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo inafikiwa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) waongeze wigo wa kufanya tafiti za maeneo ambayo maji yatapatikana sambamba na kuongeza ulinzi kwenye vyanzo vya maji ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji inatatuliwa. “Pia viongozi wa halmashauri tushirikiane kulinda vyanzo hivyo.”
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Wakaguzi wa Elimu nchini wapite kwenye shule zote wakakague vitabu vinavyotumika katika shule hizo kama vinaendana na maadili na tamaduni za Kitanzania. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameelekeza tusimamie maadili yetu, mila zetu, desturi zetu na utamaduni wetu wa Kitanzania.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 190 kupelekwa mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya sh. bilioni 47, maji sh. bilioni 30. 7, elimu sh. bilioni 32.9, nishati sh. bilioni 53.4 na barabara sh. bilioni 27.5
Comments