DC ILEJE AWAAGIZA MAAFISA UGANI KUTOA ELIMU KWA WAKULIMA
Baada ya kugawiwa pikipiki 29 Kwa maafisa Ugani wilayani Ileje mkoani Songwe mkuu wa wilaya hiyo Mhe.Farida Mgomi amewaagiza maafisa hao kuwatembelea wakulima mashambani kutoa elimu ya kilimo bora na si wakulima kuwafuata maofisini.
Mhe.Mgomi ametoa maagizo hayo Machi, 11,2023 wakati akigawa pikipiki 29 Kwa maafisa ugani wanaohudumia kata 18 zenye vijiji 71 wilayani humo hafla ambayo imefanyika katika ofisi za halmashauri ya Ileje.
Mhe.Mgomi amesema asilimia kubwa ya uchumi Kwa wananchi wa Ileje na mapato ya halmashauri hiyo hutokana na kilimo, hivyo pikipiki hizo zitumike kuwatembelea wakulima kubaini fursa na changamoto zinazowakabili Ili kuzipatia ufumbuzi.
Mhe. Mgomi amesema Kila afisa ugani kwenye eneo lake ahakikishe anatambua fursa za mazao yanayostawi kwenye kata yake na kuweka mikakati namna ya kuwawezesha wakulima waongeze uzalishaji wa mazao hayo kibiashara ili kiwainue kiuchumi.
"Pikipiki hizo hazijaja Kwa bahati mbaya bali zimekuja Kwa ajili ya kufikia 2030 kuongeza asilimia kubwa kwenye uzalishaji wa kilimo", amesema Mhe.Mgomi.
Aidha Mhe. Mgomi amesema baada ya kupata vitendea kazi ni jukumu la maafisa hao kufanya mabadiliko ya haraka ikiwepo mazao ambayo yanapatikana Kwa wilaya ya Ileje ndani ya mkoa wa Songwe ikiwepo zao la pareto, kahawa, vitunguu swaumu, Iriki, Tangawizi, viazi.
Akizungumza katika hafla hiyo mkurugenzi mtendaji wa halamashauri ya Ileje Geofrey Mnauye amesema idara ya kilimo imekuwa ikichangia ongezeko la mapato hivyo wanaamini ongezeko litakuwa la kutosha kwani wananchi watapata elimu ya kilimo Kwa mda muafaka na kuzalisha Kwa wingi.
Afisa kilimo wa wilaya hiyo Hermani Njeje amesema Ugawaji wa pikipiki hizo zitasaidia kuwafikia wananchi Kwa wakati kutoa elimu ya kilimo.
"Pikipiki hizo zimegawiwa Kwa maafisa ugani kutoka kata 18 zilizopo wakihudumia vijiji 71 hivyo wanatarajia mabadiliko ya haraka kwenye idara ya kilimo na kuongeza mapato ya halmashauri ", amesema Njeje.
Akizungumza kwaniaba ya maafisa Ugani wengine baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo afisa ugani kutoka Kijiji Cha Ikumbilo kata ya chitete wilayani humo Nuru Kashililika ameipongeza serikali Kwa kuwapa vitendea kazi hivyo na ameahidi kushirikiana na safu ya idara ya kilimo wilaya kuongeza Wigo kuhakikisha kufikia 2030 kutimizia kauli mbiu ya kilimo biashara.
Comments