MADEREVA NEW FORCE NA SAULI WAKAMATWA KWA KUFUKUZANA, DEREVA SUPER FEO ALA NDUKI KUKWEPA POLISI
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Moss Ndozero baada ya kuwanasa madereva wa mabasi ya Saulu,Super Feo na New Force wakifukuzana
Muktasari:
Mtindo wa madereva kupeana ishara ya eneo lenye askari na hivyo kupunguza mwendo umewaponza madereva wa mabasi ya Sauli, Super Feo na New Force baada ya kuwekewa mtego.
Iringa. Madereva wa mabasi ya Sauli, Super Feo na New Force wamekamatwa kwa tuhuma za kuendesha mwendo wa kasi, huku wakikimbizana baada ya Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) mkoani Iringa, Mosi Ndozero kuwawekea mtego.
Awali, Ndozero alipata taarifa za mwendo wa kasi wa mabasi hayo, hivyo akaamua kuweka mtego uliosababisha wakamatwe licha ya madereva waliokuwa wanapishana nao kuwaambia, eneo hilo hakuna askari.
Kwa sababu hawakubaini mtego huo, ishara kutoka kwa madereva wenzao zilionyesha mbele yao hakuna askari.
Akizungumza baada ya kuyakamata mabasi hayo jana Machi 29, 2023, katika Mji wa Mafinga, wilayani Mufindi, Ndozero amesema awali alipokea taarifa kwamba mabasi hayo yanakimbizana bila kujali usalama na uhai wa abiria.
Ndozero amesema licha ya kuwa kila siku madereva wamekuwa wakisisitizwa kuhusu hatari ya kuendesha mwendo wa kasi, lakini hawasikii, badala yake wanaamua kukimbizana ili kuwahi safari.
Amesema mara nyingi wamekuwa wakivunja sheria za barabarani kwa makusudi bila kujali uhai na usalama wa abiria waliowabeba.
Amewataka madereva hao kupeleka abiria waliokuwa wamewapakia hadi mwisho wa safari kisha wafike kwenye ofisi zake, Iringa mjini kuripoti wakiwa na leseni zao.
“Pelekeni abiria Mbeya mnakokwenda kisha njooni mripoti ofisini, hapa nawaambia wote leteni hamna leseni kwa hiyo kutoka Mbeya hakikisha leseni unayo mkononi hutapita Iringa. Na usije ukawasumbua abiria kwamba umezuiliwa.”
Hata hivyo dereva wa basi la Super Feo, alikimbia baada ya kubaini amefanya makosa jambo lililomlazimu dereva wa pili ashike usukani na kuendelea na safari yake.
Baadhi ya abiria waliokuwa kwenye mabasi hayo walishukuru kwa hatua hiyo wakidai kuwa madereva wengi wamekuwa wakivunja sheria, kwa kutaka kuwahi.
Comments