MALAWI WARIDHISHWA NA USHIRIKISHWAJI WA JAMII KATIKA MIRADI YA MAENDELEO WILAYANI ILEJE
Timu ya utekelezaji wa Mradi wa Bonde la Mto Songwe kutoka Wilaya ya Chitipa-Malawi imepongeza namna wananchi wanavyoshirikishwa katika mradi huo upande wa Tanzania katika wilaya ya Ileje.
Pongezi hizo zimetolewa na watalaam hao wakiongozwa na Mkuu wa msafara Mhe.MaCMillan Magomero ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chitipa wakati wa majumuisho katika Kata ya Malangali-Ileje.
Mhe.Magomero amesema kuwa maelezo waliyoyapata toka kwa wananchi tangu mwanzo katika vijiji vya Ilondo,Bulanga na Malangali yanakidhi maelezo ya mezani waliyokuwa wameyapata siku ya mwanzo katika kikao kwenye Ukumbi wa VIM.
Naye Franklin Mwalwanda Ofisa mmoja wa wageni hao ameeleza kufurahishwa kwake na namna wanawake wanavyoshikishwa katika mradi huo akisema kuwa kwa kufanya hivyo ni utekelezaji wa agenda ya kimataifa ya kuwawezesha wanawake.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe.Farida Mgomi ameshukuru viongozi wa juu wa mataifa haya mawili kwa kuruhusu ushirikiano huo kuwepo akisisitiza kuwa atasimamia na kuhakikisha mahusiano hayo yanaimarishwa zaidi ili kuwaongezea kasi ya maendeleo wakazi wa pande zote.
Ziara ya hiyo ya siku mbili imewezesha wageni kupata fursa ya kujionea namna mradi huo unavyotekelezwa katika vijiji hivyo.
Pamoja na hayo yote wajumbe wa timu ya aina hiyo kutoka Ileje wamekaribishwa Malawi lli kwenda kujifunza pia.
Wakazi wa vijiji hivyo wameelezea namna walivyojiandaa kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa chachu ya maendeleo yao na kusaidia kuulinda Mto Songwe kwa kuhifadhi mazingira.
Sister Mlungu mkazi wa Malangali amesema kuwa wamepata elimu ya kutosha juu ya uoteshaji wa miche ya kahawa wakiamini kuwa itawasaidia wao kuhifadhi mazingira pamoja na kuwaongezea kipato.
Comments