MADEREVA WA MALOLI YA MCHANGA WAANDAMANA
Madereva wa malori ya mchanga wilayani Misungwi wakijadiliana jambo kuhusu ongezeko la ushuru kutoka Sh3, 000 hadi Sh8, 000 kwa tripu moja.
Madereva malori zaidi 84 ya kusomba mchanga Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamesitisha shughuli zao na kuandamana hadi Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kupinga ongezeko la ushuru kutoka Sh3, 000 hadi Sh8, 000 kwa tripu moja.
Mwanza. Madereva malori zaidi 84 ya kusomba mchanga Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wamesitisha shughuli zao na kuandamana hadi Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kupinga ongezeko la ushuru kutoka Sh3, 000 hadi Sh8, 000 kwa tripu moja.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jumatatu Aprili 3, 2023, Mwenyekiti wa Madereva hao, Deogratius Polycup amesema ushuru huo umepanda tangu Aprili Mosi bila wao kushirikishwa.
“Hatujafahamu vigezo vilivyotumika kupandisha ushuru kwa karibia asilimia 200; kibaya zaidi ni kwamba sisi wadau hatujashirikishwa kwenye maamuzi haya yanayotuathiri moja kwa moja,” amesema Polycup
Hata hivyo, madai ya madereva hao ya kutoshirikishwa yamepingwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwu, Kashinje Machibya akisema kabla ya kupitisha maamuzi hayo, wadau wote wakiwemo madereva wa malori walishikirikishwa kupitia kwa viongozi na wawakilishi wao.
“Maamuzi ya kupandisha viwango vya ushuru ulifanyika tangu Mei, 2020 na kupitishwa na Wizara ya tamisemi lakini utekelezaji wake umeanza Aprili Mosi, 2023. Kabla ya kuyafikia maamuzi haya, viongozi wenu walishirikishwa na wakatoa maoni yao,” amesema Machibya baada ya kupokea maandamano ya madereva hao
Mwenyekiti huyo wa halmashauri amewaeleza madereva hao kuwa kwa sasa halmashauri haina uwezo wa kutengua maamuzi hayo bila kupata Baraka za Wizara ya Tamisemi.
Ameahidi kuwa uongozi wa halmashauri utashirikiana na wadau wengine wakiwemo kuzungumza na wamiliki binafsi wa maeneo ya kuchimba mchanga kuona namna ya kuwapunguzia madereva hao gharama ya kuchimba mchanga.
“Uongozi wa halmashauri pia tutafanya jitihada za kuwatafutia maeneo mengine ya machimbo ya mchanga na kuwawekea mazingira salama huku tukiendelea kujadiliana na viongozi wenu namna ya kuwapunguzia gharama," amesema Machibya
Comments