POLISI SONGWE WAOMBA USHIRIKIANO NA WANANCHI KUTOKOMEZA USHOGA NA UKATILI
Tunduma. Wananchi wa Mkoa wa Songwe wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kutokomeza vitendo vya ukatili, rushwa na ushoga vinavyoibuka katika jamii.
Rai hiyo imetolewa leo Jumapili Aprili 30, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Theopista Mallya wakati wa ziara yake aliyoifanya katika ibada katika makanisa mawili mijini Tunduma.
Kamanda Theopista amehudhuria ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) uaharika wa Tunduma na Kanisa House of Prayers lililopo pia mjini humo.
Akizungumza katika ibada hiyo, RPC huyo amesema vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili dhidi ya watoto, ushoga vimeshamiri katika jamii hivyo viongozi wa dini hawanabudi kukemea vitendo hivyo.
"Naomba tushirikiane sisi polisi na ninyi ili tuweze kuutokomeza, jambo la kwanza ni ukatili uliokidhiri katika jamii" amesema
Amesema kuwa kuna aina mbalimbali za ukatili unaofanyika katika jamii ikiwemo vipigo, ubakaji, ulawiti na matusi, unyanyasaji na unyanganyi.
"Kama nilivyosema Tunduma kuna mawimbi ya kutosha, na ninaposema ukatili ni kitu chochote ambacho ukimfanyia binadamu mwenzako kinamletea madara katika mwili au kisaikolojia" amesema
Kamanda huyo amesema kuwa kuna watu wanapiga watoto, wake na waume zao mpaka wanaua hivyo polisi wanahitaji ushirikiano kutoka katika jamii ili kutokomeza vitendo hivyo.
Amesema kuwa baada ya kufanya tafiti imebainika kuwa ulevi wa kupindukia imekuwa sababu kubwa ya vitendo hivyo vya ukatili.
Pia, amebainisha kuwa hasira, imani za kishirikina na tamaa za mali vimekuwa vikichangia matukio ya ukatili pamoja na mauaji.
Kamanda Theopista ametaja sababu nyingine inayosababisha mauaji kuwa ni wivu wa mapenzi.
Akiwa anatumia vifungu mbalimbali vya bibilia, Kamanda huyo amesema Mungu hapendi watu waonewe wala kuuawa hivyo amewasihi wenye tabia hizo kuacha.
Pia amewataka wale wenye hasira kujizuria kwa kuwa hata vitabu vitakatifu vimesema hasira hukaa ndani ya mtu mpumbavu.
"Kuna watu wanasikia kuwa fulani anampiga sana mke au mtoto lakini hawatoi taarifa, wanasema wamezoea, hakuna kuzoea ukatili, kuna watu wanaona watoto wanalawitiwa lakini hawatoi taarifa. Nilazima mtoe taarifa" amesisitiza
" Watoto wadogo Tunduma wanalawitiwa sana, wanafunzi wanatoa mimba sana, wanafunzi acheni tamaa" ameeleza
Pia, kamanda huyo ametaja jambo la pili ambalo anaomba ushirikiano kuwa ni suala la tushwa.
"Jambo la pili ni suala la rushwa. Ukimuulizia mtu yoyote hapa nani anakula rushwa atakuambia ni polisi, hata wale wanaofanya tathimini wakitaja taasisi tano polisi wapo, sasa tujiulize nani anawapa polisi rushwa?" amehoji kamanda huyo.
Amesema kama wananchi wataacha kutoa rushwa kwa polisi kutakuwa hakuna rushwa.
Amesema huduma za kipolisi ikiwemo dhamani ni bure hivyo wananchi wakiombwa rushwa watoe taarifa.
"Rushwa ni adui wa haki, anayepokea rushwa kuna haki ya mtu anaiminya, watu wanaopokea rushwa wanageuza ukweli kuwa uongo na haki kuwa dhuluma kwa hiyo ni lazima tukataze rushwa kwa sababu neno la Mungu linakataza" amesisitiza kamanda huyo huku waumini wakipiga makofi.
Amewataka waumini hao kuacha kutoa rushwa.
Jambo la tatu ambalo Kamanda huyo amelitaja ni ulawiti na ushoga hivyo amewataka wananchi kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo.
Comments