SERIKALI YASITISHA MIKOPO ASILIMIA 10 KWENYE HALMASHAURI

 Serikali imesitisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hadi hapo utaratibu mwingine utakapoelekezwa.



Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi April 13, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akihitimisha Hoja yake ya Makadilio ya Maombi na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2023/24 lakini hakusema zuio hilo linakwenda hadi lini.


Fedha za halmashauri asilimia 10 hutolewa kwa mgawanyo wa makundi matatu ambayo ni wanawake asilimia nne na vijana asilimia nne huku asilimia mbili ikiwa imetengwa kwa ajili ya kuwakopesha wenye ulemavu.


Hata hivyo, kumekuwa na kelele nyingi kwa wabunge kuhusu namna ya ukopeshaji huo ikiwemo Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambao wanasema kuwa fedha hizo zinaliwa na wajanja hata kukosa mwendelezo wake.


Leo Waziri Mkuu amesema kuanzia fedha zitakazoanza kurejeshwa mwezi Aprili mwaka huu hazitakopeshwa tena zikitakiwa kusubiri utaratibu mwingine kwa kadri itakavyoelekezwa.


Kauli ya Waziri Mkuu pia inaungana na kauli aliyoitoa hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliposema unaandaliwa utaratibu mzuri wa ukopeshaji wa fedha hizo kupitia mabenki ili kuwasaidia zaidi wahitaji.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amezungumzia suala la maadili na kuwaagiza Polisi na vyombo vingine kushughulika na watu wanaokiuka utamaduni na mila za Mtanzania kwani jambo hilo halikubariki wala kuvumilika.


Amesema serikali inafuatilia kwa karibu maeneo yote yanayoweza kuwa na uvunjifu wa maadili sambamba kufuatilia kwenye magari yanayobeba watoto wa shule ambayo yalishaagizwa kuwa na wasimamizi wakiume na kike.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE