DC ILEJE ATIMIZA AGIZO LA RAIS SAMIA
Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS wilaya ya Ileje mkoani Songwe imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya masoko ya Mbangala na Sange Kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 200 pamoja na kulipa fidia Kwa wananchi.
Kukamilika Kwa miundombinu hiyo kumepelekea mkuu wa wilaya hiyo Farida Mgomi kuzungumza na wafanyabiashara hao Mei 20,2023 kuwataka kuhamia kwenye masoko hayo kufikia Juni 24 mwaka huu.
Mgomi amesema kukamilika Kwa masoko hayo ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassani alilolitoa Julai 24, 2018 akiwa Makamu wa Rais alipofanya mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Sange.
Mgomi amesema kuhamishwa Kwa wananchi na soko la Katengele ni mpango wa Serikali kuendeleza shamba la miti Iyondo Mswima lenye jumla ya Hekta 5418 hivyo wananchi wameridhia mpango wa Serikali kuendeleza uhifadhi wa mazingira.
"Nawapongeza sana wananchi kukubali kupisha eneo hili kwani tayari Serikali ya awamu ya sita imelipa fidia kaya 11 thamani ya shilingi milioni 67,355,151 nawaombeni mkayatumie masoko mapya kuwaingizieni kipato,"amesema Mgomi.
Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi Mkuu ,shamba la miti Iyondo Mswima Jovan Emanuel amesema wakala wa huduma za misitu kwa kushirikiana na mamlaka za uthaminishaji imelipa fidia Kwa wamiliki wa vibanda vya biashara 61 zaidi ya shilingi milioni 55.
"Masoko hayo mawili yamejengwa ikiwa ni mbadala wa soko la Katengele ambapo Halmashauri wameshirikiana vyema na TFS kuhakikisha shamba la miti Iyondo Mswima linabaki salama bila kuvamiwa," amesema Emanuel.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ileje Ubatizo Songa amesema kukamilika Kwa miundombinu ya masoko hayo kutapelekea wananchi kupanga siku tofauti za kufanya biashara zao ili wajiingizie kipato.
"Tunatarajia miti iliyopandwa kwenye shamba Hilo pindi mbao zitakapoanza kuvunwa Halmashauri itanufaika kujiingizia kipato maradufu Kwa sasa kupitia zao la mbao," amesema Songa.
Akizungumza kwaniaba ya wananchi waliofika kwenye soko hilo Joseph Msokwa ameipongeza serikali Kwa maamuzi ya kujenga miundombinu ya masoko mengine na kulipa fidia Kwa wathirika hivyo agizo la kuhama eneo hilo wanalipokea ili kuanza maeneo mapya walikohamishwa kufikia Juni 23 mwaka huu.
Comments