MBUNGE WA MOMBA ATINGA NA POMBE KALI BUNGENI
Mbunge wa Momba (CCM) Condester Sichalwe ametinga bungeni na chupa za pombe kali akitaka Serikali iwasaidie wabunifu wa pombe za kienyeji ili ziweze kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Mbunge wa Momba (CCM) Condester Sichalwe ameitaka Serikali kuwasaidia wabunifu wa pombe za kienyeji ikiwemo gongo kwa kufanya utafiti na kuzifungasha vizuri ili ziweze kupata soko.
Mbunge huyo ameyasema hayo leo Ijumaa, Mei 5,2023 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka 2023/24.
“Viwanda vinaanza na mtu wa chini wa kawaida, tuheshimu mawazo yanayotolewa na watanzania wenzetu, wanatengeneza K-Vant. TBS (Shirika la Viwango Tanzania) wanaenda kupima bandarini lakini kwenda kukaa na kushirikiana na watu wa chini wawasaidie hawaendi,”alisema.
Ameitaka Serikali iwatumie wabunifu wa pombe wakiwemo ambao wamekuwa wakitengeneza vinywaji vinavyokaa siku tatu kwa kuwasaidia kuziboresha ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Najiuliza kwanini pombe za gongo zinamwagwa, ubunifu si unaanza na wazo. Sio ndio maana wanatengeneza gongo! Kwanini asipewe usaidizi wa ubunifu, kwani ubunifu unataka ni nini?” Amehoji Mbunge huyo kijana.
Amesema athari inayotajwa katika gongo ni Ethanol na Methanol lakini wapo wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambao wamefanya utafiti na kugundua hakuna madhara makubwa.
Comments