RAIS DKT SAMIA AREJESHA NYONGEZA YA MSHAHARA KILA MWAKA
Rais Samia Suluhu Hassan akipunga mkono kwenye sherehe za Mei Mosi mjini Morogoro
Licha ya ahadi lukuki walizopewa wafanyakazi leo, Rais Samia Suluhu Hassan amewaahidi kuwa Serikali inarejesha nyongeza ya mishahara ya kila mwaka ambazo zilisitishwa huku akifafanua kwanini aliweka nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa kima cha chini mwaka jana.
Dar es Salaam. ‘Wafanyakazi mambo ni moto… Mambo ni fire,’ alisikika Rais Samia Suluhu Hassan wakati akitangaza kurejesha nyongeza ya mishahara ya kila mwaka kwa wafanyakazi wa umma ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa kwa mfumo huo na Rais wa Awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli mwaka 2016.
Samia pia amewasihi wafanyabiashara kutoongeza bei madukani huku akiwaahidi wafanyakazi kuwa mambo mazuri yanakuja pasipo kutangaza hadharani nyongeza hiyo.
Mei 14 mwaka jana, Rais Samia aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambapo Sh1.59 trilioni ilitumika kwa ongezeko hilo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Wafanyakazi Iringa
Katika hotuba yake leo Jumatatu Mei Mosi, 2023 wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro Rais Samia ametoa ufafanuzi wa nyongeza hiyo.
“Mishahara kwa mwaka huu mbali na upandishaji wa posho nilizosema tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu.
“Niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona kwa mwaka huu tuzirudishe kwa wafanyakazi wote kuna nyongeza za mishahara tunaanda na tutaendelea kama tulivyokuwa tunafanya zamani,” amesisitiza.
Rais Samia amesisitiza kuwa mwaka jana Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 23.3 ambayo si kila mtu alifaidika ila lengo ilikuwa kuwainua wa kima cha chini na wengine wachache lakini kuna kindi kubwa halikuguswa.
“Nikiwemo mimi mfanyakazi namba moja. Lakini kingine tulipandisha posho za wafanyakazi na waliofaidika kwenye hili ni wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ambao hawakufaidika na ile nyongeza za mishahara ya asilimia 23.3, nafahamu kuna baadhi ya taasisi hawakuweza kulipa tulipotoa posho tayari bajeti zilishapita kwa maana hiyo mavuno yatakuja mwaka huu,” amesema Rais Samia.
Comments