WAFANYAKAZI PWANI WALIA KUKAA MAOFISI ZAIDI SAA 9 ZA KISHERIA
Baadhi ya wafanyakazi wa Mkoa wa Pwani wakiwa na mabango katika sherehe za Mei Mosi mkoani hapo, yaliyofanyika Halmashauri ya Chalinze
Chalinze. Muda wa kazi katika Idara ya Elimu Msingi ni moja ya changamoto iliyowasilishwa katika sherehe za Mei Mosi mkoani Pwani ambapo imeelezwa hauzingatiwi kwa mujibu wa sheria ya kazi namba 6 / 7 ya mwaka 2004 inayomtaka mfanyakazi afanye kazi kwa masaa tisa tu ambapo wao hufanya kazi zaidi ya muda huo.
Akisoma risala ya wafanyakazi wa Mkoa wa Pwani katika maadhimisho ya Mei Mosi, Katibu wa TUICO Mkoa wa Pwani, Neema Wilbard amesema kutokana na hali hiyo wameomba waajiri wa walimu wa shule za msingi kuzingatia sheria za kazi na kuwapa walimu stahiki zao za masaa ya ziada na pia sheria hiyo izingatiwe na waajiri ambao hawaifuati.
Changamoto zingine zilizotajwa ni baadhi ya waajiri na mashirika binafsi kukiuka sheria, kanuni na taratibu za ajira kwa wafanyakazi wao ikiwemo kutowapa mikataba, kutowalipa mishahara iliyopitishwa na Serikali kutotoa matibabu na kutowapa likizo huku wakisingizia uhaba wa watumishi.
Hata hivyo wamepongeza Serikali kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa nchini huku wakiwasihi Watanzania na wafanyakazi wote kuilinda amani ya nchi kwani hali hiyo itawezesha kuleta maendeleo nchini.
Akizungumza katika sherehe hizo kwa naiba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanal Joseph Kolombo amesema amepokea uwepo wa baadhi ya taasisi na mashirika ambayo bado hayafuati sheria za kazi kwa wafanyakazi wao ndani ya mkoa huo. Hivyo ameahidi ofisi ya afisa kazi mkoa kuyafuatilia ili kuipunguzia Serikali mzigo.
"Mimi nimepokea changamoto zote ikiwemo ya uwepo wa taasisi na mashirika yasiyotekeleza sheria za kazi mkoani hapa na zingine mlizowasilisha na nitazifikisha kwa Mkuu wa Mkoa ili zifanyiwe kazi kwa wakati," amesema Kanali Kolombo.
Pia amewataka waajiri kada mbalimbali kutoendelea kuzalisha madeni kwa wafanyakazi wao na badala yake wahakikishe wanawalipa hata yale wanayodai.
Baadhi ya wafanyakazi wamesema hali ya maisha ya Mtanzania inapanda kila siku lakini mishahara ya watumishi haiendani na hali halisi hivyo kupelekea watumishi kufanya mambo kinyume na sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi kutokana na hali ngumu ya maisha ili wajikwamue.
Katika maadhimisho hayo jumla ya wafanyakazi hodari 252 wamepewa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na zawadi, pesa taslimu, vyeti, na tuzo.
Comments