BARABARA YA ILOLO-NDOLEZI YAWAIBUA WANANCHI MBOZI
Mbozi. Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamesema ujenzi wa barabara ya Ilolo-Ndolezi utafungua fursa mbalimbali huku wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 11.01 inajengwa kwa gharama ya Sh6.46 bilioni fedha kutoka Serikali Kuu ambapo ikikamilisha itarahisisha usafiri, usafirishaji wa mazao, pembejeo za kilimo, utalii na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo barabara hiyo inapita wamesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa mkombozi kwa kuokoa gharama kubwa walizokuwa wanatumia awali hasa katika kusafiri.
Mkazi wa Kitongoji cha Mzunguko Kata ya Mlowo, Mariamu Twinzi ameeleza kuwa barabara hiyo ikikamilika watasafiri kwa gharama nafuu.
"Mimi naona barabara hii ikishakamilika tutasafiri kwa nauli nafuu. Tunamshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuona maana hii ilikuwa kama ndoto.
Tumeshaona imeshaanza kutengenezwa inaleta matumaini, natumaini sisi akinamama ambao tupo barabarani tuna vibanda tutaanza kupata wateja" amesema mama huyo.
Amesema barabara hiyo ikikamilika itawasaidia akinamama wajawazito ambao walikuwa wanapata changamoto kwenda kujifungua na wengine kujifungulia njiani kutokana na barabara kuwa na mashimo changamoto hiyo itaisha.
Pia, amesema kuwa wataweza kusafirisha mazao wakati wa mavuno kwa urahisi barabara hiyo ikikamilika.
Mwenyekiti wa wafanyabishara Mkoani Songwe Charles Chenza amesema barabara hiyo itawasaidia sana wao kusafirisha mazao yao hasa kilimo cha parachichi ambapo kwa ukanda huo kinafanyika kwa wingi hivyo barabara hiyo itawarahishia kuwafikishia wanunuzi lakini pia kuufikia uwanja wa ndege wa Songwe ili kuyasafirisha mataifa mbalimbali Dunia
Naye Mkazi wa Ilolo, Damiano Kayala amesema kuwa barabara hiyo itatatua adha ya usafiri waliyokuwa wanakumbana nayo hasa kipindi cha masika.
"Naishukuru Serikali kwa kuanza kutengeneza hii barabara, usafiri ulikuwa shida. Imekuwa bahati kuboreshwa barabara hiyo.
Hata watalii wataongezeka kwenda kuangalia kimondo kwa sababu kutakuwa na usafiri wa uhakika" amesema Damiani
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ilolo, Yahana Mwajeka amesema kuwa barabara hiyo itafungua fursa kubwa ya mji wa Vwawa na vijiji vyake kwa kuwawezesha kusafirisha mazao kwenda kwenye masoko.
"Wananchi wamefurahi sana kwani barabara hii itafungua fursa za biashara katika mji wa Vwawa.
Watatoa mazao kutoka shambani na kuyapeleka kwenye masoko" amebainisha diwani huyo.
Akizungumzia barabara hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Songwe, Lugano Mwambingu amesema barabara hiyo ambayo ujenzi wake ulianza Machi 2023 unatarajiwa kukamilikaMachi 2024.
"Tunaishukuru Serikali ya Mama Samia kwa kutoa fedha ili kutatua changamoto ya usafiriahaji wa mazao, pembejeo na wasafiri" ameeleza
Amesema barabara hiyo ni miongoni mwa barabara za mradi wa Agri Connect ambazo zinalenga kuwasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi kwenda kwenye masoko.
Mwambingu amebainisha kuwa mradi huo hauna fidia kwa wale ambao wamepisha kwa kuwa wananchi wametoa maeneo yao ikiwa ni kuunga juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo.
"Mradi huu wa barabara hauna fidia na wananchi wametoa maeneo yao na wamefurahia na kuunga juhudi za Serikali" amesema
Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo, Mhandisi Yohana Horace ametoa rai kwa wananchi kutunza barabara hiyo.
"Wananchi wanatoa ushirikiano wa hali ya juu, nitoe rai waitunze barabara hiyo" amesema

Maoni