MBOZI YAMKOSHA RC SONGWE KWA KUPATA HATI SAFI
Mkuu wa Mkoa wa Songwe (RC), Dkt Francis Michal ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa kupata hati safi iliyotokana na kujibu vizuri hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Dkt Michael ametoa pongezi hizo leo Jumamosi Juni 17, 2023 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika katika ukumbi wa Halamshauri hiyo.
Amesema kuwa alipoingia katika Mkoa wa Songwe aliweka mkazo katika suala la ujibuji hoja za CAG.
"Tunajua hoja za CAG ni kipimo cha uangalizi wa fedha za Serikali" amesema na kuongeza
"Niwapongeze sana Mkuu wa Wilaya (Esther Mahawe) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya (Abdallah Nandonde) kwa kusimamia vizuri ujibuji wa hoja za CAG" amesema.
Amesema kuwa kwa sasa mtu atakayesababisha hoja atahusika yeye mwenyewe kuzijibu.
Amewaagiza wataalamu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanajibu hoja kulingana na maelekezo waliyopewa na mkaguzi wa nje.
Amesema kuwa anawapongeza wataalamu wa halmashauri hiyo kwa kufuata maelekezo ya mkaguzi wa nje akibainisha kuwa sehemu nyingine alizopita baadhi ya wataalamu hawajafanyia kazi maelekezo waliyopewa.
Dk Michael amewataka madiwani wasiwe sehemu ya kukwamisha miradi ya maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka madiwani kuisimamia Serikali hivyo pale watakaposhindwa kuwasimamia wataalamu vizuri itasababisha kuwepo kwa hoja.
Amewasisitiza viongozi na watendaji wa Halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukasanyaji mapato na kuepuka hoja za kujirudiarudia.
Comments