POLISI WATIMBA NA MITUTU KUOKOA NDOA YA MWANAFUNZI, RC AZUIA
Mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga kidato cha tano katika moja ya shule za sekondari zilizopo Mkoa wa Tabora amenusurika kuozeshwa na wazazi wake baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme kuzuia ndoa hiyo.
Tayari wazazi wa mwanafunzi huyo wanaoishi Kijiji cha Mwawaza Wilaya ya Shinyanga walikuwa wameshapokea mahali na kupanga kumfungisha ndoa ya kimila jana, Juni 17, 2023.
Hatahivyo, lengo lao halikutimia baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akiwa anaendelea na kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samaia na wataalamu wa sheria pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo walifika kijijini hapo baada ya kupata taarifa za siri na kufanikiwa kumuokoa binti huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mndeme amesema mwanafunzi huyo ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Mwawaza mwaka jana na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano mwaka huu wazazi wake walitaka kukatisha ndoto zake kwa kumuozesha bila ridhaa yake.
Mndeme amesema kitendo hicho hakiwezi kuvumiliwa kwani kinasababisha watoto wa kike washindwe kufikia malengo yao waliyojiwekea kutokana na tamaa za baadhi ya wazazi ambao wanataka kupata mali kwa haraka jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na Serikali pamoja na jamii.
“Tukiwa katika utekelezaji wa kampeni ya huduma ya msaada wa sharia ya Mama Samia tukapata taarifa za mwanafunzi anaozeshwa na wazazi wake wameshapokea mahali siku nyingi, tukaweka mtego na kufanikiwa kuwakamata wakiwa katika harusi hiyo”amesema
Amewataka wazazi na walezi kuacha kuwaozesha watoto katika umri mdogo, kuwaacha watoto wao watimize malengo yao na siyo kutumia nguvu kudhurumu haki yao kwa kuwaozesha kwa nguvu.
John Shija, kutoka shirika la Paseshi linalojihusisha na msaada wa kisheria amelaani kitendo hicho akidai kimewasikitisha kwani Serikali inaweka mazingira mazuri ya watoto kusoma lakini bado kuna baadhi ya wazazi wanakuwa kikwazo.
Comments