RC TANGA AWAWASHIA TAA NYEKUNDU WATAKAOCHEZEA FEDHA ZA MIRADI
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amesema hatakubali kuona miradi ya maendeleo ambayo fedha zake zimetolewa ikisuasua kwa kisingizio cha ufinyu wa bajeti.
Kindamba ameyazungumza hayo jana Juni 17, 2023 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauriya Wilaya ya Korogwe lililojadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG.
Mkuu huyo wa mkoa amesema haiwezekani mikoa mingine fedha zitoshe lakini katika mkoa wa Tanga zipelee.
“Katika uongozi wangu sitavumilia kusikia miradi katika mikoa mingine fedha zimetosha na hapa naambiwa haukukamilika kwa saabu fedha hazikutosha,” ameonya.
Ameahidi kuwachukualia hatua kali wale wote ambao hawatakamilisha miradi huku akiiweka chonjo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia kwa karibu miradi hiyo.
“Unatumia fedha yote ya mradi na bado mradi haujakamilika. Inanipa shida na kujiuliza hapa Tanga kuna nini,” amesema.
Pia, amewataka viongozi wote wakiwemo madiwani na viongozi wa CCM kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuzuia vitendo vinavyokwamisha ukamilshaji wa miradi kwa wakati.
Akizungumza katika kikao hicho, Ofisa wa Ofisi ya CAG, Mwajuma Sepetu ameitaka Wilaya ya Korogwe kupitia kwa makini hoja za CAG na kuzijibu kwa nia ya kusaidia Serikali.
“Wote tunataka kuisadia serikali. Tunatoa hoja kwa ajili ya kujenga. Tuchukulie hoja hizo kama tochi tusijibu tu,” amesema.
Comments