TAKUKURU SONGWE YAWAKUMBUKA WENYE MAHITAJI MAALUMU SHULE YA MWENGE



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe imetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mwenge wilayani Mbozi.

Msaada huo wameutoa leo Ijumaa Juni 16, 2023 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ambayo inaanza leo  pamoja na maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo,  Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Edings Mwakambonja amesema kuwa wameamua kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya kujitoa kama wafanyakazi lakini na kutimiza maandiko ya Mungu ya kusaidia wenye uhitaji.


"Tumeleta zawadi mbalimbali kwa hawa watoto, tumejichangisha tukaamua tulete kwa hawa watoto kwa sababa hawa watoto ni wakwetu na wana mahitaji mengi sana hivyo tumeona walau tulete kile ambacho tumepata" amesema



Mwakambonja ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali na taasisi zisizo za kiserikali kuyasaidia makundi hayo yenye uhutaji.


"Nitoe wito kwa wadau, Mkuu wa Mkoa, wilaya na wabunge waje kuwaona watoto hawa na kuwasaidia" amesema 


Awali akisoma taarifa ya wanafunzi hao, Mkuu wa Kitengo cha wanafunzi wenye uhitaji maalumu mwalimu Eden Ngogo amesema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 108 wenye ulemavu ambapo 48 wanaishi bweni.


Mwalimu Ngogo ambaye pia ana ulemavu wa macho amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu rafiki kwa wanafunzi hao, mabweni na walimu wa elimu maalumu.


Ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kusaidia shule hiyo kutatua changamoto zinazowakabili.


Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wenye ulemavu, Emaculata Simbeye ameishukuru Takukuru kwa kuwapa msaada wanafunzi hao.


"Tunawashukuru sana kwa kututembelea leo kwa kuwa ni Siku ya Mtoto wa Afrika, tunashukuru kwa  msaada mliotuletea" amesema Emaculata ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba na mwenye ulemavu wa macho.


Mwalimu wa wanafunzi, Levina Kayombo amesema kuwa wapo watoto wengi wenye ulemavu hasa maeneo ya vijijini ambao wanafichwa na kukosa haki yao ya kupata elimu hivyo ametoa rai kwa jamii kushirikiana katika kuwapeleka watoto hao kupata elimu.


"Tunawashukuru sana wafanyakazi wa TAKUKURU kwa kututembelea, tunaomba mkawe mabalozi kwa jamii kwa kuwahamasisha kuwaleta watoto wenye mahitaji maalumu kujiunga na masomo" amesema mwalimu Levina

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE