CHADEMA WAZIDI KUVURUGANA.... WAANZA KUVUANA MADARAKA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewavua uongozi na kuwasimamisha uanachama baadhi ya viongozi wake, akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora, Lucas Kiberenge kwa kosa la kushirikiana na Hawa Mwaifunga ambaye sio mwanachama wa chama hicho.
Tabora. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewavua uongozi na kuwasimamisha uanachama baadhi ya viongozi wake, akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora, Lucas Kiberenge kwa kosa la kushirikiana na Hawa Mwaifunga ambaye sio mwanachama wa chama hicho.
Hawa Mwaifunga ni miongoni mwa wabunge wa viti maalumu 19 waliofukuzwa uanachama wa Chadema.
Akizungumza mjini Tabora leo Jumamosi Jualai 22, 2023 kwa niaba ya Kamati Kuu ya Chama hicho, Naibu Katibu Mkuu Bara Singo Kigaila Benson ametaja wengine ni mjumbe wa kamati tendaji ya jimbo la Tabora mjini na viongozi wote wa Kata ya Kakola.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa baada yakugundua viongozi hao wamepanga kushirikiana na Mwaifunga katika ziara yake jimbo la Tabora Mjini huku wakipewa siku 14 kujieleza kwa nini wasifukuzwe uanachama wa chama hicho.
Kigaila amesema licha ya kuwa kanda ya Magharibi kwa zaidi ya miezi miwili kukijenga chama hicho, waligundua Mwaifunga akifanya mikutano ya hadhara kwa kutumia jina, nembo na alama za chama jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Amekuwa akitumia jina na nembo ya chama kufanya mikutano yake jambo hili ni kinyume cha sheria,"amesema
Ameeleza kuwa, kutokana na kufanya shughuli zake kwa kutumia jina na nembo ya Chadema kinyume cha sheria atachukuliwa hatua kwa kutumia vitu hivyo wakati siyo mwanachama.
Julai 18 mwaka huu akiwa Kata ya Chemchem, Mwaifunga alifanya mkutano eneo la sanamu ya Baba wa Taifa na kusikiliza kero za wananchi bila kutumia bendera za Chadema.
Katika mkutano huo alisema yeye ni mbunge wa Taifa na wabunge wanatumia bendera ya Bunge ambayo naye aliiweka kwenye jukwaa.
Comments