DC ILEJE ACHAFUKWA USIMAMIZI MBOVU MIRADI YA BOOST. ATOA SIKU TISA KWA WASIMAMIZI KUJITATHIMINI.
Mkuu wa wilaya Ileje mkoani Songwe Mhe.Farida Mgomi ametoa siku tisa kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi mkondo mmoja katika Kijiji Cha Ikumbilo kata ya Chitete wilayani humo, huku wasimamizi wakitakiwa kujitathimini.
Mhe.Mgomi ametoa maagizo hayo Julai 21,2023 baada ya kukagua miradi ya boost katika shule ya msingi Chitete, Ikumbilo na Ilulu huku akionekana kutoridhishwa na Kasi ya ujenzi na kuagiza wahandisi wanaosimamia miradi hiyo kuweka Kambi eneo la mradi mpaka kukamilika.
Mhe.Mgomi amesema kusuasua Kwa miradi hiyo ni kunatokana na kutokuwepo Kwa usimamizi rafiki wa wahandisi kwa kuwaachia mafundi, ni baada ya kufanya ziara ya kushitukiza Kwa takribani siku mbili na kubaini mafundi kujisimamia wenyewe hali ambayo inaweza pelekea ubora wa mradi kutokidhi vigezo.
"Nimechoka na ngonjera za kutokamilika Kwa miradi hii hivyo niagize ndani ya siku tisa mradi wa shule ya msingi mpya ya Ikumbilo ukamilike, la sivyo wasimamizi msipotekeleza mtupishe", amesema Mhe. Mgomi.
"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluh Hassan imetoa fedha zaidi ya bilioni moja Kwa wilaya ya Ileje Cha ajabu mnashindwa kuzisimamia mnaonekana nyie watu wa ajabu, kuanzia sasa sitawavumilia kabla sijaulizwa mimi nitawawajibisha",ameendelea kusema Mhe.Mgomi.
Mhe.Mgomi amesema kila mtu atimize wajibu wake kuanzia ngazi ya Kijiji mpaka halmashauri, na kukemea tabia za kuwa na visingizio ambavyo havina mashiko huku akiwanyoshea vidole wahandisi kushindwa kutimiza majukumu yao.
Kwa upande wake fundi anayejenga Moja ya jengo katika shule mpya ya Ikumbilo Samweli Mbembela amemweleza mkuu wa wilaya kuwa moja ya changamoto inayowakabili ni pamoja na kuchelewa Kwa vifaa vya ujenzi hali ambayo inapelekea kutofanya kazi kwa haraka na wakati
Comments