MFANYAKAZI WA NDANI ADAIWA KUMUUA BOSS WAKE
Polisi katika Kaunti ya Kilifi nchini Kenya wanamsaka mfanyakazi wa kike wa ndani anayedaiwa kumuua bosi wake kwa kumchoma kisu na kutokomea na pesa.
Kenya. Mfanyakazi wa ndani ambaye jina lake limehifadhiwa, anatafutwa na Jeshi la Polisi nchini Kenya, baada ya kudaiwa kumuua bosi wake Rahab Karisa, kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali, siku moja baada bosi huyo kurejea nchini toka Italy.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko ya nchini humo tukio hilo limetokea alfajiri ya leo Alhamisi Julai 20, 2023, kwenye makazi ya ofisa huyo yaliyopo eneo la Mnarani Classic Estate nje ya Mji wa Kilifi.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kilifi, Fatuma Hadi, amesema wapelelezi katika eneo la tukio wamebaini majeraha ya kisu kwenye mwili wa marehemu, huku kisu hicho kikipatikana pembeni ya mwili wake.
Kesi za mikataba kimataifa zashtua wadau
Kenya hali tete, saba wapigwa risasi
"Tulitembelea eneo la tukio na kufanikiwa kupata kisu kilichotumika kuondoa uhai wa Rahab. Mwili wake una jeraha linaloonekana, lakini tunatarajia kupata majibu zaidi baada ya uchunguzi wa kitabibu kufanyika," amesema Kamanda Fatuma.
Amesema mpaka mauti yanamkuta, Karisa alikuwa Ofisa Mkuu wa Kilimo na Uchumi katika Kaunti hiyo na kwamba mwili wake uko katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kaunti ya Kilifi, ambapo uchunguzi wa kitabibu unafanyika.
“Baada ya uchunguzi wa awali kufanyika, inadaniwa kuna pesa ambazo hazionekani na inawezekana ni moja ya sababu iliyomfanya mfanyakazi huyo kumuua bosi wake,” amesema na kuongeza;
“Baada ya kutekeleza mauaji hayo, msichana huyo ametoroka na sasa anasakwa na Jeshi la Polisi ili tumfikishe katika mikono ya sheria na apate haki yake kutokana na tukio hilo.”
Comments