MTU MMOJA ALIEFUNGWA MINYORORO MGUUNI AZUA TAHARUKI MTAANI



Igunga. Mtu aliyejitambulisha kwa jina la Magai James Manyerere ameibua taharuki miongoni mwa wakazi wa mjini Igunga baada ya kuibuka mitaani akitembea akiwa amefungwa mnyororo miguuni.


Akijibu maswali ya baadhi ya watu waliojitutumua kumhoji, mtu huyo mwenye umri wa makamo amesema yeye ni mwenyeji wa Mkoa wa Mara na amefika Igunga baada ya kutoroka kutoka kwa mganga wa kienyeji alikopelekwa na ndugu zake kutibiwa ugonjwa wa kurukwa akili.


Huku akichanganya maneno kuhusu alikotoka na anakoenda, Manyerere amesema amelazimika kutoroka kwa mganga wilayani Kishapu kukwepa kunyweshwa dala za wenye ugonjwa akili.



"Ndugu zangu wakiwemo watoto wangu wanadai mimi ni kichaa; lakini siyo kweli kwa sababu mimi nina akili timamu ndio maana nimetoroka. Nataka kwenda Mwanza na baadaye nyumbani kwangu Wilaya ya Bunda,’’ amesema Manyerere


Hata hivyo, mtu huyo ambaye baadaye alichukuliwa na askari polisi kwa mahojiano zaidi hakuweza kueleza amefikaje mjini Igunga kutoka Kishapu, umbali wa zaidi ya kilometa 100.


Manyerere aliyeweza kutaja namba za simu alizodai ni za mtoto wake anayeishi mjini Bunda pia hakuweza kufafanua kwanini safari yake imemfikisha Igunga ambako ni uelekeo tofauti na njia ya kwenda mikoa ya Mwanza na Wilaya ya Bunda mkoani Mara alikodai ndiko nyumbani kwake.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha mtu huyo kuchukuliwa na askari polisi kwa mahojiano kusaisia kuwafahamu na kuwapata ndugu zake.


‘’Tayari tumefanikiwa kuwapata ndugu zake ambao wamethibitisha kuwa ana tatizo la akili na ametoroka kutoka kwa mganga alikokuwa anatibiwa; wameahidi kumfuata kesho ili kumrejesha kwenye matibabu,’’ amesema Kamanda Abwao


Amesema kwa sasa, Manyerere amepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya vipimo na matibabu wakati ndugu zake wakisubiriwa ili kupata maelezo ya kutosha kuhusu hali yake.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE