NDEGE NYINGINE YAANGUKA ZIWA VICTORIA

 Ndege ya kijeshi iliyokuwa na marubani wawili imeanguka ndani ya maji ya Ziwa Victoria, hatua chache kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba.



Bukoba. Ndege ya kijeshi iliyokuwa na marubani wawili imeanguka ndani ya Ziwa Victoria, hatua chache kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba.


Tukio hilo limetokea saa 3:30 asubuhi leo Julai 20, 2023 kuibua hofu na taharuki miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba ambao wamerejewa na kumbukumbu ya tukio la ndege ya abiria ya kampuni ya Precision Air kuanguka ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26.


Katika tukio hilo la Novemba 6, 2022 ndege hiyo ya Precision Air namba ATR 42-5H PWF ilianguka baada ya marubani kushindwa kuona njia ya kutua kutokana na hali mbaya ya hewa.




Ndege nyingine yaanguka Ziwa Victoria, marubani wanusurika

Akizungumzia tukio la leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasia Chatanda amesema ndege hiyo ya Jeshi yenye namba JW 9127 imeanguka wakati marubani wake wawili walipokuwa kwenye mazoezi ya kawaida.


Kamanda Chatanda amewataja majeruhi hao ni Leonard Nkundwa (45) na Alex Venance (30) ambapo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa matibabu.


Theophilda Kamaleki, mkazi wa mtaa wa Nyamkazi Manispaa ya Bukoba ambaye ni miongoni mwa mashuhuda wa ajali hiyo amesema mwanzoni alishuhudia ndege mbili ndogo zikizunguka na kuondoka katika anga la mji wa Bukoba kabla ya ndege moja kuonekana kuanguka ziwani.


‘’Tangu jana Julai 19, 2023 niliona ndege ndogo zikipita juu ya anga la mji wa Bukoba, leo asubuhi pia nimezishuhudia ndege hizo mbili zikipita angani kabla ya kusalia ndege moja. Baada ya muda tukapata taarifa kuwa kuna ndege imeanguka ziwani; lakini wengine wakadai ni mazoezi ya utayari wa uokoaji wakati wa ajali,’’ amesema Theophilda


Mmoja wa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Athman amesema yeye alikuwa kati ya watu wa kwanza kukimbilia eneo la uwanja wa ndege baada ya kuona ndege hiyo ikianguka ziwani lakini wakazuiwa kusogea karibu na maofisa wa jeshi waliokuwa wakifanya jitihada za kuwaokoa wenzao.


‘’Walituzuia kusogea eneo hilo mwanzoni tulijua wanafanya mazoezi lakini baadaye ikathibitika ni ajali ya kweli. Naona tayari wamefanikiwa kuivuta kutoka ndani ya maji ya Ziwa Victoria,’’ amesema Athman


Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja  vya Ndege (TCAA), Hamza Johari kupata taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo zinaendelea baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.

Comments

Popular posts from this blog

MAKONDA AWACHANA MAKAVU KATIBU CCM NA UVCCM SONGWE