NGASA AFUNGWA MAISHA KWA KUMLAWITI MTOTO WA MIAKA 4 HADHARANI
Mkazi wa Kijiji cha Madoletisa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Ngasa Polepole (19) amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Sikonge kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume mwenye miaka minne.
Hukumu hiyo imetolewa Julai 27, 2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Irene Lyatuu baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Katika shauri hilo namba 13/2023 upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi sita huku mshitakiwa akisimama mwenyewe kwenye utetezi kujitetea.
Hakimu Lyatuu amesema Mahakama imejiridhisha pasipokuwa na shaka yoyote kwamba mshitakiwa Ngasa Polepole amehusika moja kwa moja kutenda kosa hilo la udhalilishaji kwa mtoto wa miaka minne ambaye jina limehifadhiwa.
“Baada ya kupitia mwenendo wa shauri hili na ushahidi uliotolewa, Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kifungo cha maisha,”amesema
Awali Wakili upande wa Jamhuri, Joseph Mwambwalulu aliiambia Mahakama kuwa Ngasa alimchukua mtoto huyo akiwa na wenzake wawili akawapeleka porini kwenda kutafuta matunda pori, alipofika huko akatenda tukio hilo huku wenzake wakishuhudia.
Alieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mchana kinyume na kifungu cha 154 na kuiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia au wanaofikiria kutenda tendo hilo
Comments